Polisi wapambana na waandamanaji nchini Algeria
3 Machi 2019Wanafunzi hao wamefanya maandamano katika sehemu kadhaa za mji mkuu wa Algeria, Algiers kupinga jitihada za Rais Abdelaziz Bouteflika kugombea muhula wa tano katika uchaguzi ujao wa April 18.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 alipanga kujiandikisha rasmi kuwa mgombea wa kiti cha urais siku ya Jumapili kwa kuwasilisha nyaraka zake kwa tume ya uchaguzi.
Katika mji mkuu, Algiers, mamia ya wanafunzi walikusanyika katika chuo kikuu jijini Algiers na kuimba nyimbo za kuupinga mpango wa rais Bouteflika wa kutaka achaguliwe tena ili ahudumu muhula wa tano kama Rais wa Algeria.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia, polisi waliwazuia waandamanaji kutoka kwenye chuo hicho. Hata hivyo, wanafunzi wengine waliweza kupenya vizuizi vya polisi na kushiriki kwenye maandamano kuelekea katika ofisi za Baraza la Katiba, halmashauri inayoshughulikia nyaraka za wagombea katika uchaguzi huo wa rais wa mwezi ujao.
Wataka tume ya uchaguzi isipokee nyaraka zake
Waandamanaji wanaitaka halmashauri hiyo isikubali kupokea nyaraka za ushiriki za Rais Bouteflika.
Mamia ya maafisa wa polisi na wanajeshi wametawanywa kwenye mji mkuu wa Algeria na kwenye maeneo muhimu.
Maafisa hao wa usalama wameyazingira majengo ya ofisi za umma pamoja na kushika doria katika barabara kuu mjini Algiers.
Bouteflika ambaye afya yake imeendelea kudhoofika tangu alipopatwa na kiharusi mwaka 2013 anatarajiwa kuwasilisha nyaraka zake leo ambayo ni siku ya mwisho kwa wagombea kujisajili kabla ya uchaguzi wa rais wa mwezi ujao.
Maandamano yamezuka kote Algeria
Maandamano makubwa ya umma yamezuka karibu kote nchini Algeria tangu Bouteflika alipotangaza mwezi uliopita nia yake ya kuwania muhula wa tano kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Aprili 18.
Baadhi ya vyama vya upinzani vimesema vitasusia uchaguzi huo kupinga hatua ya kiongozi huyo kutaka kuchaguliwa tena kwa muhula wa miaka mitano.
Mwandishi Zainab Aziz/DPAE/RTRE
Mhariri: Rashid Chilumba