Polisi yakabiliana na waandamanaji mjini Essen Ujerumani
29 Juni 2024Msemaji wa polisi amesema kundi kubwa la waandamanaji lilifanya jaribio la kuvunja vizuizi vya polisi hatua ambayo jeshi hilo lililazimika kuwapulizia maji ya kuwasha na kutumia fimbo ili kuwadhibiti wasiendelee.
Hata hivyo haikuweza kufahamika mara moja kama kuna waliojeruhiwa. Katika mji huo wa Essen kunatarajiwa kufanyika maandamano ya hadi watu 100,000 leo hii. Mamlaka imekuwa na wasiwasi kwamba, wakati maandamano jumla yakitarajiwa kuwa ya amani, karibu watu 1,000 wenye itikadi kali za mrengo wa kushoto wangetumia njia za vurugu kuvuruga mkutano.
Takriban wajumbe 600 wa chama cha AfD wanakutana katika mji huo na viongozi wenza wa sasa Alice Weidel na Tino Chrupalla ambao wanataka kuchaguliwa tena kabla ya uchaguzi wa wabunge wa Ujerumani katika msimu wa mapukutiko mwaka ujao.