Putin, Assad wakutana Moscow
14 Septemba 2021Mkutano huo wa Jumatatu (13 Septemba) usiku ulikuwa wa kwanza baina yao tangu ule wa mwezi Januari mwaka jana uliofanyika mjini Damascus.
Televisheni ya serikali ya Syria iliuelezea mkutano huo kuwa mrefu na kwamba baadaye marais hao waliungana na waziri wa mambo ya kigeni wa Syria na wa ulinzi wa Urusi kujadiliana mahusiano baina yao na vita dhidi ya ugaidi.
Rais Assad alimshukuru Putin kwa msaada wake mkubwa wa miaka sita sasa kwenye vita vya zaidi ya muongo mmoja nchini Syria.
"Nimefurahi kukutana nawe leo hapa Moscow. Operesheni yetu ya pamoja dhidi ya ugaidi saa imeendelea kwa mwaka wa sita, ambapo ndani yake majeshi ya nchi zetu yamepata mafanikio makubwa, sio tu kwa kuzikombowa sehemu ama kurejesha wakimbizi kwenye miji na vijiji vyao, bali pia kwa kuwalinda raia wasio hatia kwenye dunia hii, kwani ugaidi haufahamu mipaka ya kisiasa na haubakii ndani ya mipaka ya kisiasa," alisema Assad.
Kwenye mazungumzo hayo, Putin alikosowa vikali kile alichokiita "uwepo wa vikosi vya kigeni" katika baadhi ya maeneo ya Syria, kauli ambayo inalenga mamia ya wanajeshi wa Kimarekani walioko mashariki mwa Syria wanakoshirikiana na wapiganaji wa Kikurdi kupambana na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu, na vile vile majeshi ya Uturuki yaliyoko kaskazini mwa Syria.
"Tatizo kubwa kwa mtazamo wangu ni kwamba vikosi vya majeshi ya kigeni bado vipo kwenye maeneo kadhaa ya nchi bila ridhaa ya Umoja wa Mataifa wala ruhusa ya nchi yako," alisema Putin.
Mageuzi ya kisiasa
Pamoja na hayo, viongozi hao wawili walijadiliana mchakato wa kisiasa wa kuirejesha Syria katika hali ya kawaida mara vita vikimalizika.
Urusi ilijiunga na vita nchini Syria mwezi Septemba 2015, wakati jeshi la Syria lilipokuwa kwenye ukingo wa kuporomoka, na tangu hapo imesaidia kurejesha nguvu na madaraka mikononi wa Assad, ambaye vikosi vyake sasa vinadhibiti sehemu kubwa ya nchi.
Uungaji mkono kijeshi na kisiasa wa Urusi kwa Syria umekuwa moja ya mambo makubwa yanayoikosanisha nchi hiyo na mataifa ya Magharibi, ambayo yameuwekea vikwazo utawala wa Moscow kwa madai ya kuupa nguvu utawala wa Assad.