Sullivan azuru Israel kuzungumzia mustakabali wa vita
14 Desemba 2023COGAT imetangaza hatua hiyo ya kusitisha mapigano kwenye ukurasa wake wa X hii leo. Hata hivyo wanasitisha mapigano hayo katika eneo la al-Salam lililoko Rafah ili kuruhusu kuingizwa vyakula na maji.
Hatua hii inafikiwa baada ya jeshi la Israel IDF kuushambulia kwa mabomu Ukanda wa Gaza. Wizara ya Afya katika eneo linalodhibitiwa na Hamas kwenye ukanda huo imesema mashambulizi hayo ya angani ya usiku mzima wa kuamkia leo yamesababisha vifo vya watu 67.
IDF lenyewe limesema jeshi lake liliwaua baadhi ya magaidi na kukamata silaha katika kitongoji cha Jabalia. Limesema, wanajeshi wake pia walifanya upekuzi katika mji wa Khan Yunis, na kuharibu mahandaki mawili, eneo la mtambo wa kufyatulia makombora pamoja na ghala ya kuhifadhia silaha.
Soma pia: Israel yashambulia Khan Younis, kusini mwa Gaza
Mwanajeshi mmoja wa IDF ameuawa kwenye mapigano na kulingana nalo, wanajeshi waliokufa hadi sasa huko Gaza wamefikia 116.
Haya yanatokea wakati mshauri wa masuala ya usalama wa taifa katika Ikulu ya White House Jake Sullivan akizuru Israel kwa mazungumzo na Netanyahu pamoja na Baraza lake la Vita.
Mchana wa leo Sullivan amekutana na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant, ambaye amemueleza kwamba vita hivyo vitachukua miezi kadhaa ya kuangamiza Hamas kwenye Ukanda wa Gaza. Gallant amesema kwamba kwa miongo kadhaa Hamas imekuwa ikiijenga miundombinu chini na juu ya ardhi na kwa maana hiyo itachukua muda mrefu kuliangamiza kabisa na kusisitiza kwamba watashinda na watasambaratisha.
Waziri Mkuu wa Ireland asema Ulaya haiwezi kuaminiwa kutokana na undumila kuwili
Wawili hao pia wamejadiliana umuhimu wa kuwarejesha Waisrael kwenye makazi yao karibu na mpaka wa Lebanon baada ya maelfu kukimbia kutokana na mapigano na wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran, hii ikiwa ni kulingana na ofisi ya Gallant.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu wa Ireland Leo Varadkar amesema hii leo kwamba Umoja wa Ulaya umepoteza uaminifu wake kutokana na kutokuwa na msimamo imara kuelekea vita hivyo na kutoa wito kwa washirika wenzake kuhamasisha usitishwaji mapigano.
Amesema hayo mwanzoni mwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya unaoiangazia Ukraine na kuongeza kuwa Umoja wa Ulaya unatakiwa kulaani ugaidi uliofanywa na Hamas, na kwa upande mwingine kutoa wito wa haki kwa watu wa Palestina.
"Tumepoteza uaminifu mbele ya ulimwengu wa mataifa yanayoendelea, ambayo kwa kweli ndio sehemu kubwa ya ulimwengu, kwa sababu ya kile kinachoonekana kuwa ni undumila kuwili. Na kuna ukweli katika hilo, kusema ukweli kabisa."
Mataifa 27 wanachama wa umoja huo kwa muda mrefu yamegawanyika kuhusiana na namna ya kuushughulikia mzozo huu na katika mkutano wao wa mwezi Oktoba walitoa tu wito wa ufikishwaji wa misaada ya kiutu huko Gaza bila ya masharti wala vizuizi pamoja na usitishwaji wa mapigano. Varadkar anasema, ana matumaini pengine safari hii watatoa tamko kali zaidi.
Soma zaidi: Nani atafadhili ujenzi mpya wa Gaza, karibu nusu ya majengo yake yamebomolewa au kuteketezwa kabisa