Rais Maduro yuko tayari kwa mazungumzo ya amani na upinzani
30 Januari 2019Kupitia mahojiano yaliyofanywa hii leo na chombo cha habari kinachomilikiwa na serikali ya Urusi, rais huyo wa Venezuela Nicolas Maduro amesema yuko tayari kukaa meza moja na upinzani kujadiliana kwa manufaa ya wananchi wa Venezuela.
Hatua hiyo inakuja wakati serikali ya Maduro imeendelea kumshinikiza mpinzani wake Juan Guaido, kufuatia mahakama ya juu kabisa nchini humo kumpiga marufuku ya kusafiri na kuamuru akaunti zake zote za benki kuzuiliwa.
Katika mahojiano hayo Maduro amepuuzilia mbali miito ya kuitisha uchaguzi mpya wa rais huku akielezea mipango ya Guaido kama mapinduzi na hatua inayokwenda kinyume na katiba.
Rais huyo wa Venezuela ameonekana akiwatayarisha wanajeshi wake wakati upinzani ukipanga maandamano mengine makubwa dhidi ya serikali yake.
Katika picha zilizooneshwa kwenye televisheni ya kitaifa, Maduro ameonekana akizungumza na wanajeshi na kuwauliza iwapo wapo tayari kuitetea nchi yao, kuiheshimu katiba na kutii amri ya amiri jeshi. Wanajeshi hao waliitika kwa sauti na kusema ndio amiri jeshi mkuu.
Juan Guaido ameendelea na mipango ya maandamano ya kumshinikiza Maduro kuondoka madarakani
Maduro amesema ni wazi Rais wa Marekani Donald Trump amepanga kumuua na kudai kwamba nia yake ni kuinyang'anya Venezuela mafuta kwa sababu nchi hiyo ina hifadhi kubwa ya mafuta ghafi kuliko taifa lolote duniani.
Lakini kwa upande wake Trump ameendelea kuwatahadharisha raia wake dhidi ya kusafiri Venezuela kufuatia mgogoro huo mkubwa wa kisiasa. Trump aliandika katika ukurasa wake wa kijamii wa twitter kwamba kuna maandamano makubwa yanayotarajiwa hii leo wamarekani wasisafiri kuelekea Venezuela hadi mawasiliano mengine yatakapotolewa.
Kiongozi wa Upinzani Juan Guaido bado anatafuta njia za kumshinikiza zaidi Nicolas Maduro aondoke madarakani. Guaido alijitangaza rais wa Venezuela na kuahidi mabadiliko. Tangu alipojitangaza viongozi kadhaa wa nchi za Magharibi pamoja na shirika la ushirikiano wa nchi za Amerika ya kusini OAS ilio na wanachama 35.
Wakosoaji wanasema uchaguzi uliofanyika mwaka uliopita uliompa ushindi maduro ulikuwa ni wa uwongo huku wakidai kuwa Maduro ameendelea kuwa na uongozi wa kidikteta.
Mwandishi: Amina Abubakar/AP/dpa/Reuters
Mhariri: Gakuba, Daniel