Republican wamteuwa Johnson kuwania uspika wa Wawakilishi
25 Oktoba 2023Johnson, mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kutokea jimbo la Louisiana, anakuwa mgombea wa nne ndani ya mwezi huu kuteuliwa kuwania kiti cha uspika, ambacho kimekuwa wazi tangu tarehe 3 Oktoba pale Kevin McCarthy alipopinduliwa na wajumbe wa chama chake walioasi.
Mgawanyiko wa ndani wa Republican umelifanya Baraza hilo kutoweza kuzungumzia vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati wala Ukraine kwa kipindi chote hiki, ama hata kuchukuwa hatua za kuzuwia kufungwa kwa baadhi ya shughuli za serikali kunakotazamiwa kuanza tarehe 18 Novemba.
Soma zaidi: Warepublican nchini Marekani wamteua mgombea wa nne wa uspika
Hakuna uhakika ikiwa Johnson ataweza kuitibu migawanyiko iliyowaangusha wenzake watatu waliotangulia kwenye uteuzi wa kuwania uspika wa Baraza la Wawakilishi kutoka ndani ya chama chake.
Katika kile kinachoashiria kuendelea kuwepo kwa migawanyiko hiyo, aliyemtangulia kwenye kura za uteuzi hapo jana, alikuwa ni spika aliyepinduliwa, McCarthy, ambaye alijizolea kura 43 hata kama hakutangazwa kuwa mgombea.
Nguvu za Trump zawaangusha
Mapema siku ya Jumanne (Oktoba 25), mjumbe wa Republican anayeshikilia nambari tatu kwenye Baraza hilo, Tom Emmer, alikuwa ndiye mshindi wa kwanza, lakini alijiondowa masaa machache baadaye kutokana na upinzani wa kundi la mrengo wa kulia kwenye chama chake.
Emmer alijitowa baada ya rais wa zamani, Donald Trump, kuwataka wajumbe wa chama chake wampinge.
Soma zaidi: Marekani: hama cha Republican chashindwa kuusuluhisha mgawanyiko ndani ya chama hicho
Tafauti na wengine kwenye Republican, Emmer alipiga kura ya kuidhinisha ushindi wa mgombea urais wa Democrat mwaka 2020, Joe Biden, dhidi ya Trump kufuatia uvamizi wa Januari 6, 2021 uliofanywa na wafuasi wa Trump dhidi ya jengo la Bunge.
Kama ilivyokuwa kwa Steve Scalise na Jim Jordan kabla yake, uwezekano wa Emmer kuwa spika ulivunjwa na kundi dogo la wawakilishi wa chama chake waliomfanya ashindwe kupata kura 217 ambazo angelizihitajia kukalia kiti cha uspika.
Mkwamo usiokwamuka
Mjumbe yeyote wa Republican, yenye viti 221 dhidi ya 212 vya Democrat katika Baraza la Wawakilishi, hawezi kupoteza kura hata nne za chama chake ikiwa anataka uspika na endapo Democrat hawakumpigia kura.
Mkwamo huu umewavunja moyo baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo, ambao wanaona kuwa siasa za ndani ya chama cha Republican zinazidi kuwa za migawanyiko.
Soma zaidi: Kevin McCarthy aondolewa kama Spika wa Bunge la Marekani
"Hatuna nafasi yoyote kwa sasa kutoa hukumu, na Baraza hili pamekuwa mahala panapohuzunisha sana kwa mtu kuwapo." Alisema mwakilishi Marc Molinaro.
Johnson, mwanasheria wa masuala ya katiba na anayefuata siasa kali za kihafidhina, amejijenga kama muunganishaji baina ya makundi yaliyogawanyika ya chama chake cha Republican.
Wilaya ya kaskazini magharibi mwa Louisiana anayoiwakilisha ni mojawapo ya masikini zaidi nchini Marekani.
Chanzo: Reuters