Robert Mugabe kuzikwa kijijini kwake Jumamosi 28.09.2019
27 Septemba 2019Msemaji wa familia, Leo Mugabe amefahamisha kwamba rais huyo wa zamani anatarajiwa kuzikwa kesho Jumamosi nyumbani kwake kijijini. Serikali kwa upande wake imesema itazingatia maamuzi ya familia. Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa alipohutubia taifa siku chache zilizopita mjini Harare alisema
Mwili wa Mugabe aliyefariki mapema mwezi huu, umehamishwa kutoka nyumbani kwake mjini Harare hadi kijijini kwake umbali wa kilometa 90 magharibi mwa mji mkuu wa Zimbabwe, Harare, kabla ya mazishi yake yanayotarajiwa kufanyika hapo kesho Jumamosi.
Baada ya majuma kadhaa ya mabishano kati ya serikali na familia ya Mugabe juu ya mahali atakapozikwa kiongozi na mwanzilishi wa nchi ya Zimbabwe, familia ya Mugabe imeamua kumzika nyumbani kwake katika kijiji cha Kutama wilayani Zvimba ambapo ndiko alikozaliwa Mugabe miaka 95 iliyopita.
Familia ya Mugabe hapo awali ilikubaliana na serikali juu ya mazishi hayo kufanyika katika makaburi ya mashujaa wa kitaifa kwenye mji mkuu, Harare, lakini baada ya kukamilika ujenzi wa kaburi la kiongozi huyo wa zamani ambalo lingelijengwa mbali na makaburi ya mashujaa wengine.
Baada ya familia kubadili nia yao, vyuma na vifaa vingine viliyoagizwa kwa ajili ya ujenzi wa kaburi hilo sasa vimerundikana kwenye eneo la kilima huku mgogoro kuhusu mahala ambapo angezikwa na kupumzishwa mmoja kati ya viongozi aliyetumikia wadhfa wake kwa muda mrefu zaidi barani Afrika ulipowa ukiendelea kuchukua sura mpya kila uchao.
Marehemu Robert Mugabe alifariki mwezi huu nchini Singapore akiwa na umri wa miaka 95. Aliiongoza Zimbabwe kwa miaka 37 kabla ya kulazimishwa kustaafu kwa kuondolewa madarakani na jeshi la nchi hiyo.
Mpwa wa Mugabe, Walter Chidakwa amesema Mugabe alifariki akiwa ni mtu aliyekuwa na masikitiko makubwa. Serikali ya Zimbabwe imesema msaada wowote wa muhimu utatolewa ili kumpa rais huyo wa zamani mazishi yanayostahili yatakayoongozwa na familia.
Mwandishi: Zainab Aziz/AP/AFP