RSF iko tayari kufanya mazungumzo na jeshi la Sudan
28 Agosti 2023RSF imewasilisha mpango uliouita "Kuzaliwa Upya kwa Sudan," unaolenga kufufua juhudi za kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na jeshi la Sudan.
Tangazo la RSF linatokea wakati mapigano kati yake na jeshi la Sudan yanaingia wiki ya 20 bila ya upande wowote kudai ushindi huku mamilioni ya watu wakiyakimbia makaazi yao.
Soma pia: Burhan ajitokeza hadharani miezi 4 tangu vita vianze
Katika taarifa iliyotolewa jana, kiongozi wa RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo alionyesha utayari wa kufanya mazungumzo na jeshi la Sudan juu ya mustakabali wa nchi hiyo.
Jeshi la Sudan na kikosi cha msaada wa dharura kwa pamoja, wameiongoza nchi hiyo tangu alipoondolewa madarakani Omar al-Bashir mnamo mwaka 2019 na kuuondoa utawala wa kiraia katika mapinduzi ya mwaka 2021.
Umoja wa Mataifa umetadharisha juu ya kutokea kwa janga kubwa la kibinadamu, baa la njaa, kusambaratika kwa huduma za afya na miundo mbinu iliyoharibika iwapo vita hivyo vitaendelea.
Pande hasimu zatuhumiana kwa kuanzisha vita
Pande hizo zinazohasimiana, RSF na Jeshi la Sudan, zimekuwa zikitupiana lawama kwa kuanzisha vita vilivyoanza Aprili 15, baada ya wiki kadhaa za mvutano juu ya kuunganishwa kwa askari wao ndani ya kikosi moja kama sehemu ya mpito kuelekea utawala wa kidemokrasia.
"Juhudi za kumaliza mzozo wa muda mrefu lazima zielekezwe kuelekea kufikia usitishaji kabisa wa vita, pamoja na uwepo wa suluhu ya kisiasa ambayo itashughulikia chanzo cha vita hivyo," ilisema taarifa ya RSF.
Chini ya mpango wake wa "Kuzaliwa Upya kwa Sudan," Dagalo ameahidi kuwa kikosi cha RSF kitaheshimu makubaliano ya awali yaliyopuuzwa kama vile kuheshimu tofauti za utamaduni, uwepo wa uchaguzi wa kidemokrasia na jeshi moja.
Taarifa ya RSF imetokea baada ya mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan kuwasili jana katika bandari ya Sudan, ikiwa ni safari yake ya kwanza nje ya mji mkuu tangu mapigano yalipozuka. Vyanzo vya serikali vimeeleza kuwa, al- Burhan atasafiri kuelekea Saudi Arabia na Misri kwa mazungumzo.
Soma pia: Wanamgambo wa Sudan wanyooshewa kidole kwa uovu
Wanasiasa wanaounga mkono demokrasia wamemuonya Burhan dhidi ya kutangaza serikali mpya, wakisema hatua hiyo huenda ikawachochea RSF kuunda serikali yao pia.
Wapatanishi wa kikanda wameonekana kuridhia uwepo wa jeshi katika serikali ya mpito.
Hata hivyo, mnamo siku ya Ijumaa, balozi wa Marekani, mmoja wa wafadhili wakuu wa kipindi cha mpito baada ya kuondolewa madarakani kwa al-Bashir, aliandika kwenye mtandao wa X kuwa, "wapiganaji hao, ambao wameonyesha kutokuwa na sifa ya kutawala, lazima wasitishe vita na kuhamisha mamlaka kwa serikali ya mpito ya kiraia."